WADAU WAKUTANA DMI KUHUISHA MITAALA
30 Aug, 2024
Wadau wa mambo ya bahari, mafuta na gesi wamekutana katika Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI) kujadili na kutoa mapendekezo ya kuhuisha mitaala ya kozi za Oil and Gas Engineering kwa ngazi (NTA Level 4-8), Mechanical and Marine Engineering (NTA Level 4-8), Maritime Transport and Supply Chain Management (NTA Leve 9) na kutoa maoni kwa mtaala mpya wa kozi ya Maritime Safety, Security and Environment Management (NTA Level 9) zinazotolewa na DMI.
Akifungua warsha hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Dkt. Wilfred Kileo aliwakaribisha na kuwaomba wadau hao kutoa mapendekezo yao kikamilifu ili kuboresha mitaala hiyo ili inapofundishwa iweze kuwasaidia wanafunzi kuwa na uwezo unaotakiwa kulingana na soko la ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara za Taaluma Dkt. Werneld Ngongi akitoa ufafanuzi juu ya mitaala hiyo minne alisema kuwa mapendekezo yote yatayotolewa yatafanyiwa kazi katika kuisaidia jamii kuelewa sekta ya bahari na maji kwa mapana na kuhamasika kwenye kuwekeza katika sekta hiyo ili kuzalisha ajira za kutosha na kukuza pato la jamii na Taifa.
Wakitoa mapendekezo wadau hao wamesisitiza uwepo wa mafunzo kwa vitendo kuanzia ngazi ya wakufunzi ili kuwawezesha kutoa mafunzo yenye uhalisia kwa vijana wanaopata elimu kutoa kwao.
Warsha za wadau hawa wanaotoa mapendekezo ya uhuishaji wa mitaala ni muendelezo wa kuhakikisha kuwa Chuo kinaendelea kuwa kituo cha ubora cha elimu na mafunzo ya bahari kwa kutoa elimu inayoendana na wakati pamoja na soko la ajira.