DMI YASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA DEHUKAM

10 Feb, 2026
DMI YASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA DEHUKAM

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Kituo cha Masuala ya Bahari na Sheria za Bahari cha Chuo Kikuu cha Ankara (DEHUKAM) cha nchini Uturuki, yakilenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya bahari na sheria za bahari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha Bahari DMI, Profesa Tumaini Gurumo, amesema makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano katika elimu, mafunzo na tafiti za masuala ya bahari na sheria zake, ikiwa ni sehemu ya jukumu la msingi la DMI la kutoa elimu na mafunzo ya bahari.

Profesa Gurumo aliongeza kuwa DMI ina dhamana ya kutoa elimu ya mabaharia pamoja na kozi nyingine zikiwemo biashara ya kimataifa na sheria za bahari, akibainisha kuwa ushirikiano na DEHUKAM utaongeza uwezo wa chuo katika kuendesha kozi na tafiti za sheria za masuala ya bahari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Masuala ya Sheria za Bahari cha Chuo Kikuu cha Ankara, Bw.Suleyman Onel, amesema ana furaha kusaini makubaliano hayo na kusisitiza kuwa ushirikiano huo utaleta manufaa kwa taasisi zote mbili na kuchangia maendeleo ya pande husika.

Naye Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dr. Bekir Gezer, amepongeza hatua hiyo na kusema kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, akisisitiza kuwa Uturuki itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha malengo ya makubaliano hayo yanatimia kwa manufaa ya pande zote.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inatarajiwa kunufaika na tafiti za sheria za bahari na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kimataifa, huku DMI ikiendelea kuimarisha nafasi yake kama chuo cha kwanza nchini kufundisha sheria za bahari katika ngazi ya uzamili.

Makubaliano ya ushirikiano yalisainiwa kati ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Profesa Tumaini Gurumo, na Mwenyekiti wa Bodi ya DEHUKAM Bw. Suleyman Onel tarehe 07 Februari 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Cha DMI.