NAIBU WAZIRI KIHENZILE AITAKA DMI KUONGEZA UBUNIFU, UTAFITI NA TEKNOLOJIA YA KISASA

16 Dec, 2025
NAIBU WAZIRI KIHENZILE AITAKA DMI KUONGEZA UBUNIFU, UTAFITI NA TEKNOLOJIA YA KISASA

 

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amekitaka Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kuongeza kasi ya tafiti bunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kutatua changamoto za sekta ya bahari na kuchochea Uchumi wa Buluu.

Akizungumza katika Mahafali ya 21 ya DMI yaliyofanyika kwenye viwanja vya  Karimjee Dar es Salaam, Mhe. Kihenzile amesema ukuaji endelevu wa sekta ya bahari unategemea rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa. Ameisisitiza DMI kuendelea kutoa elimu na mafunzo yenye ubora, ubunifu na uelekeo wa teknolojia mpya ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi.

Pia ametoa wito wa kukamilishwa kwa wakati kwa miradi ya upanuzi wa chuo  itakayoongeza upatikanaji wa elimu ya bahari kwa Watanzania wengi zaidi.

Aidha, ameelekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania wenye sifa stahiki katika miradi ya sekta ya bahari, ili kuongeza ushiriki wa wazawa kwenye uchumi wa bahari.

Akiwahutubia wahitimu, Mhe. Kihenzile amewasisitiza kutumia maarifa yao kwa ubunifu, nidhamu na bidii, akibainisha kuwa Uchumi wa Buluu ni fursa muhimu ya mageuzi ya kiuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Prof. Tumaini Gurumo, amesema DMI inahitaji meli ya mafunzo yenye uwezo wa kubeba angalau wanafunzi 200 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya mafunzo ya vitendo na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Katika mahafali haya, jumla ya wahitimu 2,076 wametunukiwa vyeti, wakiwemo 78 Shahada ya Uzamili,592 Shahada,374 Stashahada,446 Astashahada
, 538 Astashahada ya Awali
,48 Vyeti vya Umahiri (CoC). Kati yao, 512 ni wanawake sawa na asilimia 20,   ishara ya ongezeko la ushiriki wa wanawake kwenye elimu ya bahari.