Karibu
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinatoa Elimu na Mafunzo ya Bahari kwa ngazi mbalimbali ikiwemo kozi za umahiri za ubaharia yaani Certificate of competence (CoC). Kozi hizi huwaandaa wahitimu kufanya kazi ndani na nje ya nchi kutokana na ukweli kwamba Chuo kinaendesha kozi zinazotambulika kimataifa na kukifanya kiwe Kituo cha Ubora cha Elimu na Mafunzo ya Bahari katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara.
DMI imepanua wigo kutoka utoaji wa vyeti vichache vya umahiri hadi kutoa Tuzo za Ufundi (NTA) kuanzia ngazi za Astashahada hadi Shadaha za uzamili katika fani za uhandisi wa baharini, usanifu wa vyombo vya majini , Usafiri wa baharini; Usimamizi wa usafirishaji na vifaa,ununuzi, vifaa na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji na usalama wa baharini, mafuta na gesi.
Kozi za Ubaharia zinazotolewa na DMI zinasifiwa na kusimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC) chini ya mpango wa Shirika la Kimataifa la Bahari duniani (IMO), kozi za tuzo za ufundi (NTA) au Baraza la Udhibitishaji la Kitaifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET). Chuo hiki pia kina Ithibati ya kimataifa yaani ISO 9001: 2015 iliyothibitishwa na Msajili wa Kimataifa inayoitwa Det Norske VeritasGermanischer Lloyd (DNV.GL) ya kutoa elimu ya baharini na udhibitisho.
Wahitimu wanaosoma kozi zetu wanaweza kufanya kazi katika maeneo mengi kama vile mashirika ya meli, kampuni za usafirishaji, taasisi za mafunzo ya baharini, bandari, mamlaka za baharini, mashirika ya usafirishaji, mashirika ya uokozi, kampuni za utafiti wa baharini, kampuni za bima za usafirishaji, kampuni za uzalishaji wa viwandani, kampuni za madini na Utafutaji wa mafuta na gesi.
Aidha, katika kuendana na ongezeko la uhitaji wa soko katika sekta ya bahari, Chuo kimeendelea kuongeza wafanyakazi wenye uzoefu, na weledi katika kutoa mafunzo, utafiti na ushauri wa kitaalamu wa hali ya juu.
Kwa niaba ya Bodi ya Chuo, wafanyakazi na jumuiya yote ya DMI, tunapenda kukukaribisha kuungana nasi kutimiza ndoto zako katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam.
Asante.