DMI NA SHULE YA SAYANSI YA MAJINI YAJIPANGA KUSHIRIKIANA
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo leo amekutana na Mkuu wa Shule ya Sayansi ya Majini na Teknolojia ya Uvuvi (Dean-School of Aquatic Science and Fisheries Technology) Dkt. Blandina Lugendo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kuona namna ya kujenga mashirikiano na kubadilishana uzoefu katika masuala yanayohusu Bahari.
Akizungumza ofisini kwake Dkt. Tumaini amesema kuwa, amefurahishwa na ugeni huo unaolenga kukuza taaluma za Sekta ya Bahari kupitia kuanzishwa kwa ushirikiano rasmi baina ya taasisi hizo.
Ameongeza kuwa upo umuhimu wa kushirikiana kwa karibu kwa kuwa taasisi zote hizi zinashughulika na masuala ya bahari ambapo DMI imejikita zaidi kwenye shughuli zinazofanyika baharini lakini Shule ya Sayansi ya majini imejikita kwenye baiolojia.
Aidha viongozi hao wamefanikiwa pia kuzungumzia suala la kongamano la tatu la kimataifa la Uchumi wa buluu linalotarajiwa kufanyika tarehe 4 na 5 Julai 2024, linaloandaliwa na Chuo cha Bahari ambapo pia Shule ya Sayansi ya majini wameonesha utayari wa kushiriki kwa karibu katika kufanikisha kongamano hilo.