DMI NA GHANA YAUNGANA KUANDAA KONGAMANO LA TATU LA UCHUMI WA BULUU

27 Jun, 2024
DMI NA GHANA YAUNGANA KUANDAA KONGAMANO LA TATU LA UCHUMI WA BULUU

Moja ya kazi mama ya taasisi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ni kuandaa makongamano ya kitaaluma yenye lengo la kuelimisha jamii kuhusu faida ya sekta ya Bahari. Kwa kuzingatia hilo Chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chuo cha Bahari Ghana (RMU) kimeandaa kongamano la tatu la kimataifa la Uchumi wa Buluu linalotarajiwa kufanyika Julai 4 na 5 ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida zitokanazo na sekta ya Bahari.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa, ushiriki wa nchi mbalimbali katika makongamano haya unasaidia katika kujifunza na kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo ya teknolojia na masuala ya usalama ambayo ni ya muhimu katika ukuaji wa Uchumi wa Buluu.

Ameongeza kuwa nchi takribani 11 zinatarijiwa kushiriki katika kongamano hili lililobebwa na kauli mbiu ya “Kuiendea Kesho: Kujumuisha Ulinzi na Usalama wa Majini, Mabadiliko ya Tabia ya Nchi na Maendeleo ya Teknolojia kwa Ukuaji wa Uchumi wa Buluu.”

Aidha, amesema kuwa Kongamano hili linatarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko tarehe 4 Julai kuanzia saa tatu kamili asubuhi katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.

Dkt. Tumaini pia, amewakaribisha wataalamu wote waliopo kwenye sekta ya bahari, utalii, bandari, uvuvi, mafuta na gesi na wadau wote kushiriki kongamano hili ili kushiriki kikamilifu

Ikumbukwe kuwa kongamano hili linatanguliwa na makongamano yaliyofanyika mwaka 2022 na 2023.