CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) YAINGIA MASHIRIKIANO NA MAMLAKA YA UDHIBITI MKONDO WA JUU WA PETROLI (PURA).
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MOU) na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA). Hati iliyosainiwa inahusu mashirikiano ya mafunzo kwenye sekta ya mafuta na gesi ili kuweka msingi katika kuwezesha uanzishwaji wa kituo chenye ithibati kitakachotoa mafunzo ya usalama na kujihami kwa watanzania wanaofanya na wanaotarajia kufanya kazi baharini wakati wa utekelezaji wa shughuli za mafuta na gesi asilia.
Kwa niaba ya Taasisi wanazo zisimamia Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo na Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni wamesaini hati hizo za mashirikiano katika hafla iliyofanyika tarehe 13 Machi, 2024 Jijini Dar es Salaam ambapo menejimenti za pande zote mbili zikiongozwa na Wenyeviti wa Bodi zilishuhudia tukio hilo.
Mkuu wa Chuo alisema, Chuo cha bahari Dar es Salaam kina jukumu la kuandaa rasilimali watu kwa ajili ya sekta zote zinazogusa bahari, mito na maziwa. Hivyo, ushirikiano huu ni wa msingi katika kuwezesha watanzania kupata mafunzo ambayo yatawawezesha kushiriki ipasavyo katika sekta ya gesi na mafuta kwa faida ya jamii na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa kutumia wataalamu wake, Chuo kipo katika nafasi nzuri ya kuwezesha Watanzania kupata mafunzo haya ambayo yatapelekea watanzania wengi zaidi kupata sifa za kupata ajira katika miradi inayotekelezwa baharini.
Mkuu wa chuo alisisitiza kuwa, katika uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baharini suala la usalama ni la lazima kama ilivyo kwenye shughuli nyingine za baharini ambazo zinamhitaji kila anayehusika kupata mafunzo ya msingi yakiwemo ya kujiokoa, kuokoa wengine na huduma ya kwanza. Kwa kutumia wataalamu wake chuo kina nafasi nzuri ya kuwezesha watanzania kupata mafunzo yatakayopelekea watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli zinazofanyika katika maeneo ya utafutaji na uchimbaji wa gesi.
“Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni sehemu ya uchumi wa buluu. Hivyo, sekta hii ya mafuta na gesi asilia ina fursa kubwa inayoweza kuwekezwa na Watanzania. Nitoe rai kwa Watanzania kuona hizi fursa zinazopatikana baharini ili kuleta maendeleo ya uchumi wa Taifa letu” Alisema Dkt.Tumaini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa, kuanzishwa kwa kituo cha mafunzo kupitia mashirikiano hayo kutawezesha Watanzania wengi kupata mafunzo stahiki, hivyo kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za mafuta na gesi asilia zinazotekelezwa Baharini, kwani kwasasa hapa nchini hakuna kituo chenye ithibati kinachotoa mafunzo ya masuala ya usalama na tahadhari ambayo yanamlazimu kila mfanyakazi wa maeneo ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta kuyapata.
Aidha, Wenyeviti wa Bodi ya DMI na PURA walipongeza menejimenti na bodi zote kwa kuridhia mashirikiano hayo yanayolenga kukuza ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa kupitia mafuta na gesi asilia vinavyopatikana baharini.
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni (kushoto) wakibadilishana hati za mashirikiano ya mafunzo ya usalama na kujihami baada ya kusaini katika Hafla iliyofanyika tarehe 13 Machi, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni (kushoto) wakipongezana kwa kuanzisha mashirikiano ya mafunzo ya usalama na kujihami baada ya kusaini katika Hafla iliyofanyika tarehe 13 Machi, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni (kushoto) wakionyesha hati za mashirikiano ya mafunzo ya usalama na kujihami baada ya kusaini katika Hafla iliyofanyika tarehe 13 Machi, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja baina ya Uongozi wa Chuo cha Bahari (DMI) na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na timu za menejimenti baada ya kukamilisha hafla y utiji saini wa mashirikiano.
Picha ya pamoja baina ya Uongozi wa Chuo cha Bahari (DMI) timu ya Menejimenti baada ya kukamilisha hafla y utiji saini wa mashirikiano na PURA.