Watumishi wa DMI Watakiwa Kuendeleza Weledi, Nidhamu na Ubunifu Katika Utumishi wa Umma
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, amewataka watumishi wa umma kutumia taaluma, uzoefu na ubunifu wao katika kuendeleza sekta ya bahari na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza katika Mkutano wa Wafanyakazi uliofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam, Prof. Gurumo alisema kuwa ubunifu, nidhamu na uwajibikaji ni msingi wa taasisi imara na maendeleo endelevu ya sekta ya bahari.
Katika kuelekea kuhitimisha mwaka wa fedha 2025/2026, Prof. Gurumo alieleza mafanikio ya DMI katika ukaguzi wa ubora wa huduma ambapo taasisi imepata Cheti cha Ubora cha ISO 9001:2015 kinachodumu kwa miaka mitatu kupitia taasisi ya kimataifa ya DNV. Pia aliwapongeza watumishi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, nidhamu na uadilifu.
Watumishi walikumbushwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuendeleza heshima ya nchi na kujenga taswira chanya ya utumishi wa umma kwa jamii.
Aidha, Mkuu wa Chuo alizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya bahari na kuwataka watumishi kushiriki katika tafiti na bunifu zinazotoa suluhisho la kudumu kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Dkt. Lucas Mwisila, Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, alisisitiza watumishi kuzingatia taratibu za kiutumishi na kuwashirikisha wakuu wa idara na vitengo katika kushughulikia changamoto mbalimbali.
Naye Bw. Fredo Mwenyegoha kutoka Ofisi ya Uthibiti Ubora aliwataka watumishi kuendelea kutoa ushirikiano ili DMI iendelee kudumisha viwango vya ubora wa huduma vya kitaifa na kimataifa.
Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa chuo unaolenga kuwajulisha watumishi maendeleo ya taasisi pamoja na kutoa jukwaa la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taasisi na taifa kwa ujumla.
