DAMISO

Published: May 31, 2026

Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam

Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DAMISO) ni chombo muhimu kinachowakilisha maslahi ya wanafunzi na kushirikiana kwa karibu na Utawala wa Chuo katika kurahisisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya kitaaluma, kijamii na kitaifa. DAMISO hufanya kazi kama kiungo kati ya wanafunzi na uongozi wa chuo, kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kujifunzia, kuishi na kukuza vipaji vya wanafunzi.

Kupitia usimamizi na uratibu wa klabu na dawati mbalimbali kama vile Klabu za TRA, Mazingira, PCCB, TCRA pamoja na Dawati la Jinsia, DAMISO husaidia kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu masuala ya kitaaluma, maadili, uzalendo, uhifadhi wa mazingira, mapambano dhidi ya rushwa, usawa wa kijinsia pamoja na uzingatiaji wa sheria na kanuni za kitaifa. Klabu hizi zimekuwa nyenzo muhimu ya kuwajengea wanafunzi ujuzi wa uongozi, uwajibikaji na nidhamu.

Aidha, DAMISO huandaa na kuratibu semina mbalimbali za uongozi, warsha za kitaaluma na mijadala ya kielimu inayolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kitaaluma, stadi za maisha, uongozi bora, mawasiliano na maandalizi ya soko la ajira, hususan katika sekta ya bahari na usafirishaji.

Vilevile, DAMISO hushiriki kikamilifu katika maonesho ya kitaaluma ya ndani ya chuo na nje ya chuo, ikiwemo Maonesho ya Vyuo Vikuu (TCU), Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Maonesho ya Kilimo (Nanenane) pamoja na NACTVET. Ushiriki huu hutoa fursa kwa wanafunzi kutangaza programu za chuo, kuonesha bunifu na ubunifu, kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali, pamoja na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu elimu na taaluma za bahari.

Aidha, DAMISO hushiriki katika michezo ya SHIMIVUTA, mashindano ya madarasa (Interclass Competition) pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira, misaada ya kijamii na ushiriki katika matukio ya kitaifa. Shughuli hizi huimarisha mshikamano, afya ya wanafunzi, ushindani chanya na uzalendo.

Kwa ujumla, shughuli zote zinazosimamiwa na DAMISO zimechangia kwa kiasi kikubwa kutangaza, kuinua na kuimarisha taswira ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kitaaluma, kijamii na kitaifa, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza rasilimali watu, maendeleo ya elimu ya bahari na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.