WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR AIPONGEZA DMI KWA KUANDAA WATAALAMU WENYE UJUZI KATIKA SEKTA YA USAFIRI KWA NJIA YA MAJI

18 Aug, 2026
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR AIPONGEZA DMI KWA KUANDAA WATAALAMU WENYE UJUZI KATIKA SEKTA YA USAFIRI KWA NJIA YA MAJI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, amekipongeza Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa mchango wake katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi na umahiri unaohitajika katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji.

Mhe. Lela amesema hayo alipotembelea banda la DMI tarehe 26 Julai wakati wa kufunga Maonesho ya 7 ya Wiki ya Elimu ya Juu Pemba.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Chuo kuendelea kuzalisha wataalamu bora wenye uwezo wa kujiajiri na kuchangia katika kukuza uchumi wa buluu.

Chuo cha Bahari Dar es Salaam kilishiriki maonesho hayo ikiwa ni sehemu ya kusogeza huduma karibu na wananchi wa Pemba. Kupitia banda lake, chuo kimetoa elimu kuhusu fani mbalimbali za sekta ya usafiri kwa njia ya maji zinazotolewa chuoni, kutoa ushauri wa uchaguzi wa fani kulingana na ufaulu wa waombaji, pamoja na kusajili waombaji papo kwa papo kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

Kupitia ushiriki huo, DMI imeendelea kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu fursa za elimu na ajira katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa buluu nchini.