WATAALAMU WATAKIWA KUJIKITA KWENYE TAFITI SEKTA YA UCHUMI WA BULUU ILI KUENDANA NA DIRA YA MAENDELEO 2050

Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amewaelekeza wataalamu sekta ya Uchukuzi pamoja na Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI) kujikita katika tafiti zitakazoibua uwekezaji kupitia sekta ya uchumi wa buluu ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Maelekezo hayo ametoa leo Jijini Dar es salaam wakati akifunga kongamano la kitaifa la uchumi wa buluu lililoandaliwa na Chuo cha Bahari cha Dar es salaam (DMI), Chini ya Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Profesa Khyarara amesema uwepo wa Bahari, Mito na Maziwa nchini Tanzania ni fursa muhimu katika kukuza pato la taifa hivyo ni lazima wataalamu wajipambanue katika kufanya tafiti pamoja na kuchambua maeneo muhimu ambayo yataleta tija na kuleta uhimilivu toshelezi wa uchumi.
Akizungumzia maazimio yaliyotokana na kongamano hilo Mkuu wa Chuo cha Bahari cha Dar es salaam (DMI) Profesa Tumaini Gurumo amesema kuwa maazimio hayo ni, wadau wa uchumi wa buluu kuandaa mipango ya utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu, matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu yazingatie uhimilivu wa mazingira kwa maendeleo endelevu.
Prof. Gurumo ameongeza kuwa ni muhimu kuandaa mpango wa utoaji elimu na mafunzo ya uchumi wa buluu kuanzia ngazi za elimu ya awali kwani, kama nchi imeamua kuwa uchumi wa buluu ni miongoni mwa sekta zinazoenda kukuza pato la taifa ni vyema kujenga uelewa kwa watoto kuanzia ngazi za elimu ya awali.
Pia, kuongeza uwekezaji wa makusudi katika tafiti na bunifu zinazochochea uchumi wa buluu, kuhakikisha ushiriki jumuishi kwa vijana na wanawake katika sekta zote za uchumi wa buluu ili kutengeneza taifa tunalotarajia uchumi wa buluu endelevu pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yote ya maji.
Kongamano hili la siku mbili kuanzia tarehe 10 hadi 11 limefungwa leo huku likiwakutanisha Wadau mbalimbali wa Uchumi wa Buluu kutoka taasisi za Serikali na Binafsi ambapo limebebwa na kauli mbiu isemayo Bahari Yetu, Fursa Yetu, Wajibu Wetu.