WANAFUNZI WANNE (4) WA DMI WAPATA UFADHILI KWENDA KUSOMA KOREA

04 May, 2023
WANAFUNZI WANNE (4) WA DMI WAPATA UFADHILI KWENDA  KUSOMA KOREA


Uongozi wa Chuo Cha Bahari Dar es salaam (DMI) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Korea ya Kusini leo umewapatia wanafunzi wanne (4) kutoka chuo cha bahari Dar es Salaam ufadhili wa kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo melini (Global on Board Training) katika Chuo Cha Korea Maritime and fisheries institute kilichopo nchini Korea kusini.

Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo amesema uhusiano bora kati ya nchi mbili Tanzania na Korea Kusini umeleta matokeo haya ya wanafunzi kupata Ufadhili wa kwenda kupata mafunzo kwa vitendo.

Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo amewaasa wanafunzi wanaokwenda nchini Korea kwaajili ya mafunzo hayo kutumia fursa vyema na kuweka jitihada kwenye mafunzo ili kupata ujuzi bora utakaoweza kulisaidia Taifa na Chuo katika kukuza sekta hii ya bahari.

“Nafasi hii ya kupeleka wanafunzi 4 ni kubwa sana kwetu, ukizingatia chuo hiki cha Korea huchukua watu 40 tu kwa mwaka Duniani, hatuna meli lakini chuo kinajitahidi kutafuta wadau watakaoweza kusaidia wanafunzi wetu kupata ujuzi wa Kimataifa, tunaishukuru sana Serikali kwa ushirikiano na mataifa haya”Alisema Dkt.Gurumo

Kwa upande wake aliyekua Mkuu wa Chuo Cha Bahari Mhandisi Thomas Mayagilo amesema tukio lilofanyika ni zuri na linaleta tija katika Taifa kwa kuongeza idadi ya wataalamu nchini, aidha ameiomba Serikali iongeze nguvu katika sekta ya bahari kwakua fursa ni nyingi sana.

Wakishukuru wanafunzi wa Chuo Cha Bahari Dar es salaam, kwa kupata fursa ya kwenda nchini Korea ya Kusini kupitia chuo Cha Bahari Dar es salaam wametoa shukrani zao za dhati kwa Serikali pamoja na uongozi wa Chuo na kuahidi kujituma kwenye mafunzo yao.

Mafunzo haya ya vitendo ndani ya meli yanatarajia kuchukua muda wa miezi mitatu ndani ya meli wakijifunza mambo mbalimbali hususani katika uongozaji wa vyombo vya majini.

Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo akipokea zawadi ya shukurani kwa ushirikiano aliuonesha kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo

Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo akizungumza kwenye ukumbi wa Mikutano wa DMI, Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo na kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo Utawala,Fedha na Mipango.

Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo akiwa ameongozana na Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo wakitoka kutazama madhari ya Chuo.

Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam  na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda mafunzoni Korea.

Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo (katikati) kulia ni Makamu wa Chuo Fedha Utawala na Mipango Dkt.Wilfred Kileo, na kushoto ni Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Dkt.Luca Mwisila wakimshukuru Balozi wa Korea ya Kusini na Msaidizi wake kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha.

Aliyekua Mkuu wa Chuo Cha Bahari Mhandisi Thomas Mayagilo akizungumza maoni yake kwa Serikali juu ya kuboresha Sekta ya Bahari Nchini.

Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt.Tumaini Gurumo, akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi waliopata fursa kwenda kupata mafunzo ya vitendo Melini Nchini Korea.

Wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam  wakiwa tayari kwa kuondoka.