WANAFUNZI WA DMI WAZIDI KUNG'ARA KOREA

17 Sep, 2024
WANAFUNZI WA DMI WAZIDI KUNG'ARA KOREA

Wanafunzi 5 kutoka chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) wapo nchini Korea ya Kusini wakipata mafunzo miezi mitatu ya vitendo Melini. Mafunzo hayo  ni Sehemu ya Mafunzo ya ubaharia ambapo   wanapata uzoefu na sifa ya kufanya  mitihani ya mahojiano  kabla ya kupata vyeti vya kuwawezesha kufanya  kazi kwa nafasi  za Maofisa wa unahodha  na uhandisi kwenye meli za kitanzania na za Kigeni.

Wanafunzi waliondoka Mwezi Augosti  mwaka huu na wanatarajia  kuhitimisha mafunzo yao mwezi Novemba mwaka 2024.

Mkuu wa Chuo cha DMI Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa mafunzo hayo wanayopata katika meli za chuo cha Korea Institute of Maritime and Fisheries Technology (KIMFT) yanawasaidia wanafunzi  kupata uzoefu wa kufanya kazi kwenye meli zenye mabaharia kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni.

 “Chuo chetu cha DMI kinaushirikiano na chuo hiki cha Korea (KIMFT) hivyo wanafunzi wetu wamepata fursa ya mafunzo ya kuhudumia meli huko. Chuo cha KIMFT kina meli nne za mafunzo, tofauti na huku kwetu, pia kule wanakutana na wanafunzi kutoka nchi za Indonesia, Vietnam, Philippines, Thailand , Peru na Fiji” alisema Dkt Tumaini.

Wilfrida Ngallu ni Mwanafunzi anaepata Mafunzo ya Uhandisi wa Meli, anasema kuwa  mafunzo hayo yanawasaidia kupata uzoefu wa kufanya kazi katika Meli na kujifunza tamaduni za mataifa mbalimbali.

Wanafunzi wanaopata mafunzo hayo kutoka DMI  ni Wilfrida Ngallu, Rachel Mwijaruba, Glory Mrema, Neville Lohay na Ahmad Selele, kwa upande wa  Uhandisi wa meli pamoja na Unahodha. Hii ni  awamu ya pili kwa chuo cha DMI kupeleka wanafunzi nchini Korea kupata Mafunzo  katika Meli. Awamu ya kwanza chuo kilipeleka wanafunzi 4 ambapo wote walifanya vizuri na kupata mikataba ya kufanya kazi kwenye meli za nje ya nchi.