WAHITIMU WA VETA LEVEL III NA D MBILI ZA KIDATO CHA NNE WAKARIBISHWA DMI KUONGEZA WIGO WA AJIRA

Ili kupanua wigo wa ajira wa kufanya kazi nchi kavu na baharini wahitimu kutoka vyuo vya VETA ngazi ya Level III ya kozi za welding, mechanical, electricity na fabrication na wenye ufaulu wa kuanzia masomo mawili (D 2) katika mtihani wa kidato cha nne wamehamasishwa kujiunga na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Akizungumza kwenye maonesho ya miaka 50 ya VETA yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Mkufunzi wa DMI, Nahodha Emmanuel Nanyaro, amesema sekta ya bahari inakua kwa kasi na kiwango Cha Elimu na mafunzo yanayotolewa chuoni yanawawezesha vijana kufanya kazi duniani kote.
Nahodha Nanyaro amesema wapo baadhi ya wanafunzi waliosoma VETA kisha kujiunga na DMI kusoma elimu ya ubaharia ambao wamepata fursa ya kufanya kazi nje ya nchi kama wachomeleaji na mafundi umeme kwenye meli.
"Tunatoa wito kwa vijana wanaosoma VETA wakimaliza wasiishie tu kule nchi kavu waje Chuo cha Bahari wapate elimu ya baharini, wajifunze ufundi mitambo wa baharini wajue injini za meli namna ambavyo zinafanya kazi na kozi nyinginezo,” Amesema Nahodha Nanyaro
Aidha katika maonesho hayo Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo kikuu Huria Mhe. Mizengo Peter Pinda ni miongoni mwa viongozi waliotembelea Banda la Chuo Cha Bahari Dar es salaam alifanikiwa kupata maelezo mafupi kuhusu Elimu na Mafunzo yanayotolewa na Chuo Cha Bahari Dar es Salaam, Uchumi wa Buluu na namna Wanafunzi wanaohitimu VETA wanaweza kujiunga na Kozi za Ubaharia zitakazo wawezesha kufanya kazi melini ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa ajira.
Chuo Cha Bahari Dar es salaam kimeshiriki maonesho hayo yaliyohitimishwa tarehe 22 /03/2025 kutoa Elimu kuhusu uhusiano uliopo baina ya kozi zinazotolewa DMI na VETA ikiwa ni sehemu ya kukuza wigo wa ajira za wahitimu nchini.