MABAHARIA WAMETAKIWA KUWA MABALOZI WA KULINDA NA KUTUNZA MAZINGIRA YA MAJI NA KUELIMISHA JAMII UMUHIMU WA KUTUNZA BAHARI NA MAZIWA
Tuunge mkono juhudi na kuwa mabalozi wazuri wa kulinda mazingira ya maji ili yaweze kututunza sisi pamoja na rasilimali zinazopatikana katika maji.
Ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassa Masala alipokuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Amosi Makalla kwa kufungua Warsha ya wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji na Mabaharia leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza.
Mhe. Hassan alisema kuwa wadau wote waliokusanyika kwenye warsha hiyo hususani Mabaharia wanatakiwa kuwa chachu katika kutekeleza mkataba wa MARPOL kwa kulinda mazingira ya bahari na maziwa wakati wote wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na kuhakikisha juhudi zinaendelea kufanyika ikiwemo kutoa elimu mbalimbali za kutunza mazingira ya maji.
Aidha alitoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza na viunga vyake kuhakikisha wanatunza mazingira ya Ziwa Victoria kwa kutokutupa taka hovyo, kuzuia uvuvi haramu wa kutumia sumu na baruti, badala yake kuwa mabalozi katika kuhakikisha Ziwa linakuwa safi ili kuchochea ukuaji wa viumbe hai waliopo majini.
Akitoa neno la shukurani Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt.Tumaini Gurumo alisema kuwa anashukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa mapokezi mazuri waliyotoa, Mchango mkubwa wa Serikali katika kutia moyo fani ya mabaharia, kwani anaiona sapoti ya viongozi katika maadhimisho hayo kuwa ni baraka katika kutekeleza yale yote yaliyopangwa hadi kufikia kilele yaani tarehe 25, Juni.
Warsha ya wadau wa Sekta ya Usafirshaji kwa njia ya Maji leo waliweza kujadili masuala mbalimbali kwa mustakabali wa maendeleo ya Uchumi wa Taifa kwa ujumla, huu ni muendelezo wa miongoni mwa shughuli za maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani yanayofanyika Jijini Mwanza.