MAADHIMISHO YA SIKU YA MABAHARIA DUNIANI YATUMIKE KUJADILI HALI ZA MABAHARIA KWA USTAWI WA KUKUZA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII.

23 Jun, 2023
MAADHIMISHO YA SIKU YA MABAHARIA DUNIANI YATUMIKE KUJADILI  HALI ZA MABAHARIA KWA USTAWI WA KUKUZA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII.

Serikali imewataka wadau wa Sekta ya Uchukuzi kwa njia ya maji Nchini kutumia fursa ya maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani kujadili na kutafakari juu ya hali za mabaharia na mustakabali wa ustawi wao katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame (Mgeni rasmi) ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha vilivyopo Jijini Mwanza kuanzia Tarehe 22 mpaka 25 Juni,2023.

“kazi ya ubaharia siyo uhuni kama wengi wanavyochukulia, hii ni kada yenye weledi wa kutosha na wataalamu mahili ambao wana taaluma na wamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na Dunia kwa asilimia zaidi ya 80 katika Sekta ya usafiri kwa njia ya maji.

Mhe. Makame aliongeza Kwa kusema kuwa Mabaharia wengi wao wameendelea kuishi maisha magumu kutokana na mishahara duni, mazingira magumu ya kazi na kutokuwa na mapumziko wala likizo kwa mabaharia wanaoajiliwa na baadhi ya Wasafirishaji binafsi.

Aidha, amesema Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mhe. Dkt Hussein Ally Mwinyi zimeweka kipaumbele kuwekeza katika miundombinu na vyombo vya usafiri majini kama vile ukarabati wa meli ya Mv Umoja, ujenzi wa Meli mpya ya Mv mwanza bara na kuridhia ununuzi wa meli mbili mpya na ukarabati wa meli ya Mv mapinduzi kwa upande wa Zanzibar ambavyo vitasaidia kukuza ajira za mabaharia na kukuza uchumi huku zikihakikisha maslahi ya mabaharia yanalidwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi kutoka Chuo Cha Bahari Dar es Salaam Kapt.Ernest Bubamba alisema kuwa , Chuo Cha Bahari ambacho ndicho wazalisahji wakuu wa Mabaharia Nchini kitaendelea kutoa Elimu na Mafunzo yenye viwango Kwa kuzingatia Mikataba na Miongozo ya Mabaharia.

Kapt.Bupamba ameushukuru Uongozi wa Wilaya ya Ilemela Kwa kutoa eneo kubwa la Ujenzi wa tawi la Chuo Cha Bahari Mwanza, ili kurahisisha utoaji huduma ya Elimu na Mafunzo kwa wananchi wa Mwanza na maeneo jirani.

Maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani 2023 yamebebwa na kauli Mbiu ya "Miaka 50 Mkataba wa Kimataifa wa kuzuia Uchafuzi wa Mazingira ya Bahari unaotokana na Meli (MARPOL) Uwajibikaji wetu Unaendelea".

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame  akitoa maelekezo kwa Chuo kusimamia asili yake ya mafunzo alipotembelea banda la Chuo cha Bahari kwenye maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame akipokea ufafannuzi wa kitaaluma unaotolewa Chuoni  kutoka kwa Injinia Danford Mlay, Mkufunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam.

 

 

 

Injinia Danford Mlay akitoa ufafanuzi kuhusu Chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa wageni waliotembelea banda la Chuo kwenye maonesho ya  maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani.

Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Capt.Ernest Bupamba akizungumza na wageni waliohudhuria ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani.

Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Capt.Ernest Bupamba  akijitambulisha kwa wageni waliohudhuria maadhimisho ya siku ya Mabaharia Duniani.

Wenyeviti wa Bodi na baadhi ya wakuu wa Taasisi kwenye picha ya pamoja wakati wa ufunguzi wa siku ya mabaharia Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya furahisha Jijini Mwanza.

Kamati ya maandaliizi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni rasmi pamoja na meza kuu.