VIJANA WAKIKE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZILIZOPO KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI.

25 Jun, 2023
VIJANA WAKIKE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZILIZOPO KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala , akisoma taarifa ya kufungwa kwa maadhimisho ya siku ya mabaharia Duniani leo kwenye viwanja vya Furahisha Jijini mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amesema kuwa, Takwimu za Shirika la Bahari Duniani (IMO) zinaonesha Mabaharia Duniani kote, wanafikia Milioni Moja na laki Sita (1,600,000) ambapo kwa Tanzania tuna Mabaharia takribani elfu tisa (9,000), kati ya Mabaharia  Wanawake ni pungufu ya asilimia moja (yaani 0.6%), hivyo anatoa wito kwa vijana wa kike kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Akizungumzia utekelezaji wa mkataba wa MARPOL Mhe. Hassan amesema kuwa , Mabaharia ni kiungo muhimu katika kutekeleza Mkataba  wa kulinda mazingira ya bahari na maziwa kwa kuwa muda wote wapo kwenye vyombo hivyo wakifanya shughuli za uchukuzi na kuvuna Rasilimali za Majini. Hivyo anawakumbusha kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini Mkataba wa MARPOL mwaka 2004 wa vyombo vya usafiri majini kulinda Mazingira ya Bahari, unaozuia vyombo vya usafiri majini kumwaga Mafuta, kutupa taka mbalimbali ikiwa ni pamoja na takasumu ambazo ni hatari kwa Afya ya Binadamu na Viumbe wanaoishi majini.

Aidha amesema,Serikali  ya Tanzania inaendelea kutatua changamoto zilizopo katika Sekta hii ya usafiri Majini kwa kuwa inafahamu wazi kuwa asilimia tisini (90%) ya Biashara yote ya Kimataifa Duniani inabebwa na Meli. Hivyo basi, itambulike kuwa mchango wa sekta ya Usafiri majini ni mkubwa zaidi, ukilinganishwa na njia zingine za usafirishaji Kitaifa na Kimataifa na hiyo inamaanisha kuwa  Mabaharia ndio nguzo muhimu katika kukuza Uchumi wa Dunia na Tanzania kwa ujumla.

Akitoa neno la shukurani Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Kapt.Ernest Bupamba amesema kuwa anamshukuru Rais kwa kuamua kukarabati meli zote ambazo zilikuwa zimesimama na Kutengeneza  Meli kwenye maziwa Makuu yote nchini kwani, Chuo cha Bahari Dar es Salaam kimejiandaa kuzalisha Mabaharia Wataalamu kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa ili kukidhi  mahitaji na soko la ajira.

‘’Niwaombe wakazi wa Mwanza na Maeneo Jirani msisite kuleta watoto wenu Chuo cha Bahari, Serikali imedhamiria kuimarisha usafiri kwa nia ya maji hivyo ajira mabaharia watahitajika, DMI ndio mahali pekee tunapozalisha wataalamu hawa, hivyo niwakaribishe sana” Alisema Kapt.Bupamba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maandalizi ya maonesho hayo Bi.Stella Katondo (Mkurugenzi Idara ya Usalama  na Mazingira –Uchukuzi) amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatambua na kuthamini Mchango wa Mabaharia si tu kwakuandaa maadhimisho bali kupitia mikata inayosainiwa inayolenga kusimamia haki na maslahi yao wawapo kazini na hata baada ya kustaafu,Nchi yetu inaukanda mkubwa sana uliozungukwa na maji  hivyo tunavyoendelea kujiweka vizuri kimataifa kwa kuwazalisha mabaharia wenye viwango kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa  kufuata Mkataba wa IMO tutaiwezesha Nchi yetu kuwa bora Kiuchumi na Kijamii.

Kilele cha Siku ya Mbaharia Duniani kiliambatana na utoaji tuzo kwa Mabaharia wawili waliofanya matendo ya kishujaa na mbio za marathoni ambapo Jumla ya Taaasisi nane kutoka Tanzania Bara na Visiwani zimeshiriki maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani ikiwemo Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), wazalishaji wakuu wa Mabaharia Tanzania na ukanda wa kati wa Afrika.