UCHUMI WA BULUU NI FURSA, WATANZANIA JITOKEZENI KUCHANGAMKIA.

27 Jun, 2023
UCHUMI WA BULUU NI FURSA, WATANZANIA JITOKEZENI KUCHANGAMKIA.

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Mhe.Suleiman Masoud Makame, amewaasa Watanzania kujitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa ya Uchumi wa Bluu kupitia rasilimali zinazopatikana Baharini.

Waziri amesema hayo leo Juni 27 jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua kongamano la pili la Uchumi wa Bluu kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).Aidha, amekitaka Chuo Cha Bahari kutoa Elimu ya kutosha Kwa jamii kuhusu fursa zitokanazo na Maji ili kuikomboa Tanzania kiuchumi.

Waziri Makame amesema uchumi wa bluu ni mwarobaini wa umasikini wa Watanzania, kwani asilimia 75 ya usafirishaji wa vitu vinasafirishwa kwa njia ya bahari na ndiomaana hata Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Dkt.Hussein Ali Mwinyi wamewekeza nguvu Kubwa katika kukuza dhana ya Uchumi wa Bluu kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo , Kapteni Ernest Bupamba, amesema Kongamano hili linalenga kuelimisha wadau na wananchi kuhusu maana ya uchumi wa bluu na rasilimali zinazopatikana kuipitia uchumi wa bluu kama vile utalii, usafirishaji, mafuta na gesi na namna gani watazifaidi.

"Sisi kama DMI kazi yetu ni kuaanda wataalamu ambao wataisaidia Serikali katika eneo hili la Uchumi wa Bluu ,tumeanza mchakato wa kujitanua zaidi ili tuweze kuwafikia wengi na tunashukuru Serikali inatuunga mkono mfano kwa sasa tunatarajia kujenga matawi Mwanza eneo la Ilemela na Lindi tawi litakalohusika kuandaa wataalamu wa ujenzi wa boti" alisema Kapt.Bupamba

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)Dkt.Tumaini Gurumo amesema kongamano hili linakutanisha wadau na watanzania kwa ujumla katika kujadiliana jinsi gani wanaweza kuzipambanua fursa hizi za uchumi wa Bluu kwa jamii lakini pia kuchochea uwekezaji unaopatikana katika maeneo ya bahari, mito na maziwa tuliyonayo ikiwemo Usafirishaji, Uvuvi na Utalii unaohusiana na maji.

Akizungumzia kuhusu utoshelevu wa Wataalamu Dkt.Tumaini amesema bado hawajatosheleza na kutoa rai kwa vijana wa Kitanzania kujitokeza kusomea fani za masuala ya maji kwani, Chuo kimejitosheleza katika kuzalisha rasilimali watu kwenye eneo la usafirishaji kwa njia ya maji na kinaendelea kuanzisha kozi mbalimbali ili kupata wataalamu wabobezi watakaofiti kwenye sekta hii ya Uchumi wa Bluu.

Kongamano la Uchumi wa Bluu ni la siku moja ambapo limeambatana na uwasilishwaji wa mada kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam.