WATAALAMU WA USAFIRISHAJI MUHIMU KUONGEZA USHINDANI WA BIDHAA ZA TANZANIA

18 Aug, 2026
WATAALAMU WA USAFIRISHAJI MUHIMU KUONGEZA USHINDANI WA BIDHAA ZA TANZANIA



Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema kuongeza wataalamu katika usafirishaji, lojistiki na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa bidhaa ni muhimu katika kuongeza tija, ushindani wa bidhaa za Tanzania na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Prof. Gurumo ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane leo tarehe 08, 2026, yaliyohitimishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Viwanja vya John Malecela Nzuguni, Dodoma.

Amesema kilimo na usafirishaji vina uhusiano mkubwa, kwa kuwa mazao yanayozalishwa yanahitaji mifumo bora ya usafirishaji na lojistiki ili kuwafikia walaji na masoko kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika.

“Tunapozungumzia biashara shindani au uchumi shindani, maana yake si kushindana ndani ya nchi pekee, bali tunautazama ushindani wa kimataifa,” amesema Prof. Gurumo.

Amesema DMI inaendelea kuboresha mitaala, vifaa vya kufundishia na mafunzo kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia, ikiwemo mifumo ya kidijitali na Akili Bandia (AI), ili kuandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Katika kilele hicho, Prof. Gurumo alipata fursa ya kutembelea mabanda ya Wizara ya Uchukuzi, ikiwemo banda la DMI, Wizara ya Uchukuzi na kujionea shughuli mbalimbali pamoja na huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Kupitia Maonesho ya Nanenane, DMI imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na vijana kuhusu fursa za elimu, mafunzo na ajira katika sekta za bahari, usafirishaji na lojistiki.