TARATIBU, KANUNI NA MIONGOZO YASISITIZWA KUZINGATIWA KATIKA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZA USAFIRI MAJINI
Wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji wametakiwa kuzingatia taratibu, sheria, kanuni na miongozo ya ndani na nje ya nchi katika kuendesha shughuli zao ili kulinda usalama wa usafiri kwa njia ya maji.
Rai hiyo imetolewa leo na Mhe. Makame Machano Khaji, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya usafiri kwa njia ya maji duniani na miaka 50 ya Tanzania kuwa mwanachama wa IMO yanayofanyika kwenye viwanja vya Mkendo Wilayani Musoma Mkoani Mara kuanzia tarehe 23 hadi 26 Septemba, 2024.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mhe. Makame amesema ni muhimu kuzingatia mkataba wa kuzuia uchafuzi wa mazingira ya Bahari, Mito na Maziwa kwani usafiri wa maji ni muhimu katika ukuaji wa uchumi kwa kuwa asilimia 80 ya bidhaa zote duniani hutumia usafiri huu.
Naye Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo amesema, DMI kinatoa mafunzo kwa mabaharia na wataalamu wanaofanya kazi kwenye sekta ya maji kwa ujumla, kupitia kauli mbiu iliyobebwa na maadhimisho ya sherehe hizi, Chuo kinapaswa kutazama mabadiliko ya sekta ya Bahari nchini na duniani hususani mabadiliko ya tabia nchi ili kukabiliana ipasavyo na uchafuzi wa mazingira.
Ameongeza kuwa, Chuo kinatazama teknolojia mpya na ubunifu katika kuendesha vyombo vya usafiri majini ili kuhakikisha usafiri kwa njia ya maji unakua salama na kuendeleza suala la kuzuia uchafuzi wa mazingira kwani usipozingatiwa uchumi pia utatetereka.
“Musoma kwetu ni fursa, tutatoa elimu na mafunzo kwa siku hizi chache na kuhamasisha vijana kujiunga na Chuo ili kuzalisha rasilimali watu ambao watafanya kazi kwenye bahari, mito na maziwa tuliyonayo badala ya kutumia wataalamu kutoka nje ya nchi” alisema Dkt. Gurumo.
Maadhimisho haya ambayo kilele chake hufanyika Alhamisi ya mwisho wa mwezi wa tisa kila mwaka. Mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Navigating the Future: Safety First” na kwa tafsiri isiyo rasmi ni “Mustakabali wa Uendeshaji Vyombo vya Usafiri Majini: Usalama Kwanza”.