WANAFUNZI KUTOKA CHUO CHA BAHARI (DMI) WASHIRIKI ZOEZI LA KUCHANGIA DAMU SALAMA.

10 Jan, 2023
WANAFUNZI KUTOKA CHUO CHA BAHARI (DMI) WASHIRIKI ZOEZI LA KUCHANGIA DAMU SALAMA.

 

Wanafunzi kutoka chuo cha bahari dar es salaam wameshiriki zoezi la kuchangia damu kupitia foundation ya NIFUATE  iliofanikisha zoezi la kuchangia damu kupitia mfuko wa taifa wa damu salama ambapo pia Wanafunzi wamepewa  elimu juu ya umuhimu uchangiaji damu.

Mkurugenzi wa foundation ya Nifuate Joshua Haruna Zayumba  akizungumza na wanafunzi chuoni hapo alisema  kwamba, Taasisi hiyo imejikita kusaidia watu wenye Ulemavu, Yatima, waathirika wa dawa za kulevya na pia kusaidia kutoa damu salama. pia amewashukuru sana wanafunzi kwa kuchangia damu salama na kuwasihi wanafunzi wawe na moyo wa kusaidia.

Katibu mkuu mtendaji wa nifuate foundation Mwita Thomas Kibugili amesema kua leo ni siku ya furaha kwao kwasababu wamepokea ugeni kutoka Wizara ya Afya kupitia kitengo cha damu salama kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa damu salama ambapo , ameshukuru uongozi wa chuo cha DMI kupitia ofisi ya mshauri wa wanafunzi  kwa kusaidia kufanikisha zoezi la uchangiaji damu.

Afisa mhamasishaji mpango wa Taifa damu salama kanda ya mashariki Bw.Joeli Emmanuel Temba amesema wamekuja kukusanya damu kwa ajili kupeleka kuokoa nguvu kazi ya taifa ya wamama wajawazito, wahanga wa ajali, watu wenye ugonjwa wa moyo n.k.

“ kwakweli nimeona faraja kwa  wanafunzi hawa kwa namna walivyojitolea kutoa damu kwa lengo la kuwasaidia wenzetu wenye uhitaji, naomba kuwahamasisha  kwamba waendelee na moyo huo wa kujitolea”.

Afisa kutoka mpango wa taifa wa damu salama Bi.Salma Jumanne Ramadhani akizungumzia  sifa za mchangia damu amesema kwanza lazima mtu awe na Afya njema, Asiwe kwenye dozi ya dawa, Asiwe na ugonjwa wa kudumu mfano homa ya ini,presha na maambukizi ya ukimwi. Pia amesema baada ya kuchangia damu mtu hatakiwi kufanya mazoezi, kutembea umbali mrefu na pia ameshauri anywe maji kwa wingi.

Aisha Rashidi  mwanafunzi wa chuo cha DMI amesema anashukuru Nifuate Foundation na uongozi wa chuo kuendesha zoezi hilo na amehakikisha amechangia damu siku ya leo ,pia anashauri wengine wale ambao wanasifa ya kuchangia damu waweze kufanya hivyo kwani Damu tunaweza kuihitaji wakati wowote.

Noeli Zakaria Mfisi mwanafunzi kutoka chuo cha bahari anasema jambo la kutoa damu ni jambo jema na kubwa kwasababu tunasaidia kuokoa maisha ya watu wengine, kwamba amepokea wito chanya wa kutoa damu hivyo anashukuru amepata fursa hiyo.

Katika kampeni ya kuchangia damu salama wanafunzi 50 wameweza kuchangia damu salama itakayoweza kwenda kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji wa damu.

Mwanafunzi wa DMI akipata maelekezo ya kufuata kabla ya kuchangia damu kutoka kwa Mkurugenzi wa foundation ya Nifuate Joshua Haruna Zayumba  

Mwanafunzi wa DMI akiwa kwenye zoezi la uchangiaji damu salama

 

Mwanafunzi wa DMI akichukuliwa vipimo kabla ya zoezi la uchangiaji damu salama kuanza.

 

Mwanafunzi wa DMI akiwa kwenye zoezi la uchangiaji damu salama

 Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi DMI wakiwa katika picha ya pamoja na wageni waliofika kuhamasisha zoezi la uchangiaji damu salama.