SERIKALI YAOMBWA KUISAIDIA DMI MELI YA MAFUNZO KWA VITENDO

04 Dec, 2023
SERIKALI YAOMBWA KUISAIDIA DMI MELI YA MAFUNZO KWA VITENDO

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bahari Zanzibar, Bi.Sheikha Mohamed ameiomba Serikali kukiwezesha Chuo Cha Bahari Dar es salaam kuwa na Meli ya Mafunzo kutokana sehemu kubwa ya Elimu inayotolewa kuwa ya vitendo zaidi ya nadharia.

Akifungua Kongamano la pili la kitaaluma kwenye ukumbi wa DMI tarehe 29/11/2023 Mkurugenzi amesema kuwa, Chuo kinazidi kukua, na fani hii ni ya Mafunzo Kwa vitendo zaidi, hivyo wakati umefika wa Chuo kuwa na Meli yake ili kuzalisha wataalamu watakaoendana na teknolojia katika sekta ya Bahari.

Ameongeza kuwa katika kufungua fursa za Uchumi wa Buluu mbali na kuwa na Meli ya vitendo pia ni vyema chuo kujikita katika nyanja zingine katika kufungua fursa na kwamba upo umuhimu kwa serikali kukitazama Chuo Kwa jicho la pili katika kukiwezesha ili fursa zitakazofunguliwa ziweze kuendana na teknolojia.

" asilimia kubwa ya wataalamu wanaofanya kazi kwenye sekta hii ya maji ni Wanafunzi kutoka Chuo hiki, na niseme, vijana wapo vizuri na wanaweredi , natoa Rai Kwa Chuo kuhakikisha kinaenda sambamba na Fursa hizi kama za utalii, uvuvi, michezo ya Baharini na eneo la mafuta na gesi." Alisema Mkurugenzi.



Naye Mkuu wa Chuo Cha Bahari Dar es salaam Dkt Tumaini Gurumo amesema kuwa Kongamano hilo ni sehemu ya kusherehekea kazi inayofanywa na Chuo yaani ya kutoa Elimu na mafunzo ya Bahari.

Amesema kuwa Kongamano hilo limewakusanya wadau na wanafunzi waliowahi kupata Elimu na Mafunzo chuoni (Alumni) ili kuwasikia ni Kwa kiwango gani wamefanikiwa, mitazamo na maoni yao juu ya maendeleo ya Chuo na uboreshaji wa huduma inayotolewa.

Aidha Dkt.Tumaini amewakaribisha watanzania wote kuja kupata Elimu na mafunzo katika Chuo Cha Bahari kama kauli mbiu inavyosema kufungua fursa za Uchumi wa Buluu, uliolenga ushirikishaji wa watanzania katika kujipatia faida ya kiuchumi kupitia matumizi Bora ya maji yaliyopo kwenye Bahari, Mito na Maziwa.

KONGAMANO la pili la kitaaluma liliambatana na utoaji wa tunzo Kwa Wanafunzi Bora, wadau wanaoshiriki kuchukua Wanafunzi wa Chuo Cha Bahari kwenye Mafunzo ya vitendo na wakufunzi walioshiriki kuandika maandiko mbalimbali.