USALAMA WA MABAHARIA NA ABIRIA NI KIPAUMBELE KATIKA KUENDELEZA SEKTA YA USAFIRI MAJINI – MHA. ALI BAKAR
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mha. Ali Said Bakar, kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Khalid Mohamed amesema Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa mabaharia na abiria pamoja na kuendeleza sekta ya usafiri majini kwa maendeleo ya Taifa.
Mha. Bakar ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yanayofanyika mkoani Kigoma kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026, yanayoongozwa na kaulimbiu isemayo “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora katika Sekta ya Usafiri Majini.”
Mha. Bakar amesema usafiri majini una mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuunganisha wananchi na kuwezesha biashara, hivyo Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya sekta hiyo, kuongeza ujuzi wa mabaharia na kusimamia usalama.
Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za udhibiti na wadau wa sekta hiyo katika kupunguza ajali za majini na kuhakikisha matumizi salama ya vyombo vya usafiri majini na kuwaasa mabaharia kuzingatia maadaili ili wasitumiwe kinyume na kazi zao.
Katika ziara yake kwenye mabanda ya maonesho, Mha Bakari alipata fursa ya kutembelea banda la DMI na kupokea taarifa kuhusu majukumu ya chuo, huduma za elimu na mafunzo zinazotolewa kwa jamii pamoja na mchango wa DMI katika kukuza uchumi wa Buluu.
Aidha, Mha Bakari alikipongeza chuo cha DMI kwa kazi bora inayofanya katika kutoa elimu ya ubaharia pamoja na kukuza vipaji vya mabaharia hususani vijana wa sasa.
DMI inashiriki maonesho haya kama madau mkubwa katika sekta ya bahari na kinatumia maonesho haya kuhamasisha vijana na wadau mbalimbali kujiunga na program za masomo katika ngazi ya Cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili pamoja na Kozi za kitaaluma za Cheti cha Umahiri kwa Mabaharia (CoC), kufuatia kufunguliwa rasmi kwa dirisha la udahili kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
DMI inawakaribisha wakazi wote wa mkoa wa Kigoma na maeneo ya jirani kutembelea banda la DMI katika maonesho haya ili kupata elimu na kuzijua fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya bahari.


