DMI: MAFUNZO YA BAHARI YAIMARIKA KIMATAIFA

28 Jul, 2023
DMI: MAFUNZO YA BAHARI YAIMARIKA KIMATAIFA

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimeendelea kuimarisha ushirikiano na mataifa ya nje katika kutoa mafunzo ya vitendo melini kwa wanafunzi wake.

Aliyasema hayo Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Dkt. Tumaini Gurumo katika hafla ya kuwapokea wanafunzi waliotoka nchini Korea ambao walipata nafasi ya mafunzo kwa vitendo katika chuo cha bahari Korea (Korea Institute of Maritime and Fisheries Technology) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Korea uliopo nchini Tanzania.

Dkt. Tumaini Gurumo amesema kupitia ushirikiano huo, chuo cha DMI kimefungua fursa kwa wanafunzi wake kupata mafunzo nchini Korea na siku zijazo chuo cha DMI kinatarajiwa kusaini mkataba wa makubaliano (MoU) na chuo hicho.

Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa chuo cha DMI kitaendelea kukuza ushirikiano wa ndani na nje ya nchi, amewaomba mabalozi wa nchi zingine zenye fursa za mafunzo melini kusaidia upatikanaji wa nafasi kwa vijana wa kitanzania ili kuzalisha wataalam wenye weledi katika tasnia ya bahari.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Kapt. Ernest Bupamba amemshukuru Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Togolani Mavula kwa ushirikiano aliouonesha wa upatikanaji wa nafasi za mafunzo kwa vitendo melini (Seatime taraining) kwa wanafunzi wanne wa DMI kwenye Chuo cha Bahari nchini Korea.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Janeth Phares ameshukuru serikali ya Tanzania na Korea na uongozi wa chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa kuwaamini kuwakilisha nchi na chuo katika mafunzo ya melini nchini Korea.

Wanafunzi hao wapatao wanne waliondoka nchini Tanzania tarehe 4/05/ 2023 na kurejea Tanzania tarehe 27/07/2023.