PROF. GURUMO AITANGAZA TANZANIA KIMATAIFA KUPITIA SEKTA YA BAHARI
Mchango wa Watanzania katika kuendeleza sekta ya bahari kimataifa umezidi kutambuliwa baada ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Shabani Gurumo, kutunukiwa tuzo ya heshima ya Mwanafunzi wa Zamani Mashuhuri (Outstanding Alumna Award) kutoka Chuo Kikuu cha World Maritime University (WMU), kilichopo nchini Sweden.
Tuzo hiyo imetolewa kutambua mchango wake katika kuimarisha uongozi, elimu na mafunzo ya sekta ya bahari, pamoja na kuchochea maendeleo ya taasisi zinazohusika na sekta hiyo barani Afrika.
Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Bwana Arsenio Dominguez, alimkabidhi Prof. Gurumo tuzo hiyo Oktoba 31, mwaka huu, wakati wa mahafali ya 43 ya WMU yaliyofanyika nchini Sweden.
Prof. Gurumo ana zaidi ya miaka 20 ya uzoefu katika sekta ya bahari, akiwemo miaka 10 katika nafasi mbalimbali za usimamizi na uongozi. Amechangia maendeleo ya sekta hiyo kupitia ufundishaji wa sheria za bahari, utafiti na kuimarisha uwezo wa wataalamu katika maeneo ya bandari, usafirishaji wa majini na masuala ya bahari.
Akizungumzia mchango wake, Rais wa WMU, Prof. Maximo Mejia Jr., amesema Prof. Gurumo ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya kitaaluma kuendeleza sekta ya bahari kupitia ufundishaji, utafiti na ushauri wa kitaalamu.
Prof. Gurumo pia ni mtafiti na mwandishi wa machapisho mbalimbali, ikiwemo kitabu kinachohusu Uchumi wa Buluu, fursa na chachu ya maendeleo. Aidha, amekuwa mshauri wa kitaalamu katika masuala ya uchumi wa buluu na usafirishaji wa majini kwa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) na TradeMark East Africa (TMEA).
Kupitia mchango wake, Prof. Gurumo amesaidia kuboresha elimu na mafunzo ya sekta ya bahari, kuimarisha viwango vya ubora na kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi katika meli, bandari na mamlaka za usimamizi wa bahari na usafirishaji wa mizigo.
Katika mahafali hayo, Watanzania wengine wanne walitunukiwa vyeti vya kuhitimu shahada ya uzamili na stashahada katika fani mbalimbali za sekta ya bahari.
Mafanikio hayo yanatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa na kuongeza nafasi ya Tanzania katika maendeleo.
