SEKTA BINAFSI ZICHANGAMKIE FURSA ZA UCHUMI WA BULUU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa wito kwa Serikali na sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Uchumi wa Buluu kwa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu, ujuzi na rasilimali watu, ili kuongeza ajira, uwekezaji na matumizi endelevu ya rasilimali za majini.
Mhe. Masauni amesisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za bahari na maji kwa njia endelevu, akieleza kuwa teknolojia, maarifa na uwekezaji ni muhimu katika kubadilisha rasilimali hizo kuwa fursa halisi za kiuchumi. Ametoa wito huo leo, Septemba 7, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akifungua kwa niaba ya Makamu wa Rais Kongamano la 5 la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Kongamano hilo linafanyika kwa siku tatu, Septemba 7–9, 2026, likiwakutanisha watunga sera, watafiti, wawekezaji na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha maendeleo ya Uchumi wa Buluu barani Afrika. Kaulimbi ya Kongamano ni "Kuwezesha Shughuli za Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika.”
