KAMATI YA BUNGE YAFURAHISHWA NA UWEKEZAJI WA VIFAA VYA MAFUNZO KWA VITENDO DMI, YAAGIZA UJENZI WA KAMPASI MPYA

18 Mar, 2026
KAMATI YA BUNGE YAFURAHISHWA NA UWEKEZAJI WA VIFAA VYA MAFUNZO KWA VITENDO DMI, YAAGIZA UJENZI WA KAMPASI MPYA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kufurahishwa na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kufundishia kwa vitendo (simulators) katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), uwekezaji ambao umeendelea kuongeza ubora wa mafunzo na kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya sekta ya bahari.

Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi chuoni hapo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, aliipongeza Serikali kwa juhudi hizo, akieleza kuwa vifaa hivyo ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo ya kisasa yanayolingana na viwango vya kimataifa.

Kutokana na umuhimu na mchango wa chuo hiki katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya bahari nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kamati hiyo imeielekeza Wizara ya Uchukuzi kusimamia ujenzi wa Chuo katika eneo jipya la makao makuu ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI). Hatua hiyo inalenga kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kisasa itakayolingana na hadhi ya chuo hicho kikongwe na cha kipekee nchini.

Mhe. Kakoso alibainisha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha vifaa vya kufundishia, mazingira na majengo ya sasa ya chuo hayalingani na hadhi na mchango wake katika sekta ya bahari. Alieleza kuwa DMI ni chuo pekee cha aina yake nchini kinachohudumia pia nchi za Afrika Mashariki, hivyo ni muhimu kipate eneo la kutosha litakalowezesha upanuzi wa miundombinu, utoaji wa mafunzo kwa uhuru zaidi pamoja na kuvutia wanafunzi wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Akipokea maelekezo hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alieleza kuwa Serikali imelipokea suala hilo na mipango ya utekelezaji ipo tayari. Alibainisha kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) itajenga kampasi mpya ya DMI katika eneo la Kimbiji. Alisema hatua hiyo itakipa chuo mazingira bora ya kisasa na wakati huo huo kutoa nafasi kwa Bandari ya Dar es Salaam kujitanua katika eneo la sasa la chuo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Prof. Tumaini Gurumo, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji unaoendelea chuoni, hususani katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya mafunzo kwa vitendo ambavyo vimeongeza thamani na ubora wa elimu inayotolewa.

“Tunaishukuru sana Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia. Vilevile, tunaishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa maelekezo mahsusi na yenye manufaa kwa chuo kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na kuendeleza viwango vya kimataifa,” alisema Prof. Gurumo.

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinaendelea kujidhatiti katika kutoa wataalamu mahiri wa sekta ya bahari ili kukuza na kuendeleza Uchumi wa Buluu nchini na barani Afrika.