KAMATI YA USTAWI WA JAMII BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR WAKIPONGEZA CHUO CHA DMI.

Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wametembela Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa lengo la kujifunza ili waweze kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inayolenga kujenga Chuo cha mabaharia Visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mitambo na vifaa vya kujifunzia na kufundishia, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Sabiha FilFil Thani amesema kuwa anaushukuru uongozi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa ushirikiano waliotoa, kwani wamefanikiwa kujifunza kuhusu namna ya kuendesha Chuo cha Bahari, Pamoja na kuwa na vifaa vya mafunzo vitakavyowezesha kutoa elimu bora pamoja na taaluma kwa wakufunzi watakaotarajiwa kuwa waalimu wa chuo hicho.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Ali Abdul-Gulam Hussein amesema, ziara imekua ya umuhimu mkubwa kwa kutembelea Chuo cha DMI ambacho kimetangulia katika taaluma za ubaharia. Ziara pia itawasaidia kuepuka makosa wakati wa ujenzi wa chuo kipya na kamati itaishauri ipasavyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hususani katika eneo la vifaa vya kujifunzia na kufundishia ambavyo vina gharama kubwa itakayolazimu Serikali kuwekeza fedha nyingi.
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Prof. Tumaini Gurumo amesema kuwa chuo kimefanikiwa kuwaeleza shughuli zinazofanyika hasa eneo la kozi za ubaharia zinazosimamiwa na mkataba wa kimataifa unaojulikana kama STCW 1978 ambao unalazimu Chuo kuwa na Wakufunzi wabobezi katika maswala ya ubaharia, vifaa vya kujifunzia na kufundishia vinavyojulikana kama Simulators ambazo ni nusu ya uhalisia wa baharini na wanafunzi wa ubaharia kufanya mazoezi ya uhalisia baharini.
Ameongeza kuwa Chuo cha DMI kinasimamiwa na taasisi za kimataifa na kitaifa ambapo kimataifa DMI inasimamiwa na taasisi iliyothibitishwa na shirika la Kimataifa la Bahari Duniani IMO inayojulikana kama Det Norske Veritas (DNV) inayotazama viwango vya ubora vya elimu inayotolewa chuoni. Kitaifa, Chuo kinasimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kupande wa mitaala inayotolewa kwa mabaharia
“Katika kukidhi matakwa ya kitaifa na kimaifa chuo tumefanikiwa kuongeza mitambo ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia inayolenga kuhakikisha viwango vya ubora vya elimu vinavyoendana na maendeleo ya teknolojia ambapo itawalazimu chuo tarajiwa cha Zanzibar kufuata matakwa hayo. Alisema Prof Tumaini.
Chuo cha DMI ni chuo pekee kinachotoa mafunzo ya ubaharia hapa nchini na chuo kinachotambulika kitaifa na kimaifa. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekiwezesha chuo kupata mitambo ya kisasa kama vile Full Mission Engine Room and Bridge Simulator, GMDSS Simulator, High Voltage Simulator, Lathe Machine na Drilling machine kwa lengo la kuboresha utoaji elimu.