HIFADHINI VIUMBE NA KULINDA MAZINGIRA YA BAHARINI - DKT. BITEKO

04 Jul, 2024
HIFADHINI VIUMBE NA KULINDA MAZINGIRA YA BAHARINI - DKT. BITEKO

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kulinda viumbe vya baharini na kuhifadhi mazingira ya bahari kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.

Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati akifungua kongamano la Tatu la Uchumi wa Buluu mwaka 2024 lenye kaulimbiu: Kuunganisha Usalama Baharini, Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Teknolojia kwa ajili ya Ukuzaji wa Uchumi wa Buluu

Amesema uchumi wa buluu unatambuliwa kama mchangiaji mkubwa wa maendeleo endelevu ambapo jamii hutumia rasilimali za bahari kwa njia ambayo ni endelevu na kwa kiasi kikubwa huzingatia uhifadhi wa mazingira.

Ameongeza kuwa uchumi wa buluu huchochea uvumbuzi wa fursa  kama vile teknolojia ya kibayoteknolojia na nishati ya bahari, kutoa suluhu za nishati mbadala na tiba, ambazo husaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ulinzi wa mifumo ikolojia, na kuhakikisha  Ulinzi na usalama wa bahari ambao ni muhimu kwa usalama wa usafiri wa majini na kuzuia shughuli haramu baharini. 

"Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ibara ya 136 (e) imeelekeza, kuibua na kuendeleza Sekta  mpya za uchumi ikiwemo uchumi wa buluu (blue economy), ubunifu (creative industry) na uchumi wa kidigitali. Uchumi wa buluu  ni shughuli zote za kiuchumi zinazohusiana bahari na maziwa makuu pamoja na rasilimali zake," amesisitiza Dkt. Biteko.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema uchumi wa buluu ni uchumi mtambuka unaohusisha sekta mbalimbali. Amesema kongamano hilo limekua chachu katika kutoa fursa na mafunzo  kwa watanzania katika Sekta ya bahari.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema mkoa wa unahusika kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa buluu. Amewataka wadau kuendelea kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu.