WAHITIMU WATAKIWA KUTUMIA TAALUMA YAO KUINUA UCHUMI WA TAIFA

27 Dec, 2022
WAHITIMU WATAKIWA KUTUMIA TAALUMA YAO KUINUA UCHUMI WA TAIFA

 

Serikali imewataka wahitimu wa kozi mbali mbali za Sekta ya bahari nchini kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kushauri namna bora za kutumia fursa zilizopo kwenye uchumi wa bluu unaotokana na sekta ya bahari ili kuinua pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Akizungumza katika mahafali ya 18 ya Chuo cha bahari Dar es Salaam (DMI) Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema uchumi wa bluu unawategemea sana wataalam waliohitimu kozi za bahari hasa ukizingatia kuwa sasa Serikali inawekeza katika ujenzi wa miundombinu na meli katika bandari zetu.

 

“Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya bandari pamoja na ujenzi wa meli katika maziwa yetu yote hii ni katika kutekeleza azma ya kutumia fursa za uchumi wa buluu, hivyo mliohitimu tambueni kuwa Serikali inawategemea sana ‘ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na uwekezaji huo kwenye miundombinu ameutaka uongozi wa DMI kuhakikisha inaainisha changamoto zilizo ikiwemo za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi ili Serikali iongeze nguvu kwenye eneo hilo kwa maslahi mapana ya kuongeza ujuzi kwa vitendo kwa wanafunzi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba amesema Chuo kimeendelea kuongeza kozi katika maeneo mbalimbali ambapo mpaka mwaka 2022 kimeweza kuongeza kozi za shahada ya uzamili kufikia tano kutoka kozi tatu zilizokuwapo kwa mwaka 2021.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa chuo Dkt. Tumaini Gurumo ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa simulator mbili ambazo zitasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo kabla ya kuingia baharini.

Katika mahafali ya 18 Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amewahudhurisha wanafunzi zaidi ya 900 wa kozi mbalimbali wakimemo wa shahada ya uzamili, shahada, astashahada na cheti.

Mhe. Atupele Mwakibete (MB),Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mgeni rasmi katika Mahafali ya 18

Meza kuu wakiimba wimbo wa Taifa

Wahitimu

Dkt. Tumaini Gurumo,Kaimu Mkuu wa Chuo – DMI

Kapt. Ernest Bupamba, Mwenyekiti wa Bodi – DMI