ELIMU YA UVUVI SALAMA YAWAFIKIA WAVUVI WA LINDI
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) tarehe 19 Agosti kimezindua kampeni inayolenga kutoa elimu ya usalama baharini na shughuli za uvuvi kwa wavuvi wa Lindi ikiwa imebebwa na kauli mbiu ya “Uvuvi Salama kwa Ustawi wa Jamii”
Akizungumza na viongozi wa wavuvi na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Lindi kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Sea View Beach Resort, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa, Chuo kimeanza kutoa elimu hii kwa wavuvi wa Lindi kwa sababu Lindi ina ukanda wa pwani mkubwa zaidi ukilinganisha na maeneo mengine kama Mtwara na Tanga.
Dkt. Tumaini ameongeza kuwa Soko la samaki ni kubwa ndani na nje ya nchi. Vilevile, amesema kuwa vijana wa kitanzania wenye sifa wana uwezo wa kuchukuliwa kufanya kazi kwenye meli za uvuvi za nchi ya Jamhuri ya Korea kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi zetu.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema kuwa kampeni imekuja kwa wakati muafaka kwani wavuvi wa Lindi wamekuwa wakihitaji elimu kama hii ili kuwawezesha kubadili fikra za uvuvi wa kimazoea na kugeuza kuwa fursa inayoweza kuzalisha ajira kwa vijana wengi hasa kwa kuzingatia urefu wa ukanda wa Bahari ya Hindi.
“Uvuvi wa hapa ni wa kurithi sio wa kitaalamu. Kama ambavyo mmekuja kutoa hii elimu, niwasisitize wale watakaofanikiwa kufikiwa kwa kipindi hiki kutumia vyema fursa hii kujifunza yale wasiyoyafahamu ili kuelewa usalama wa shughuli za uvuvi na bahari kwa ujumla na kutumia vema shughuli za uvuvi katika kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na pato taifa” alisema Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake msimamizi wa Kozi fupi kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam Mhandisi Deism Mlay amesema kuwa, kozi za uvuvi zitakazotolewa ni za aina tatu yaani Kozi za usalama baharini kwa wavuvi, Kozi za unahodha wa vyombo vya uvuvi vyenye ukubwa tofauti na Kozi ya usalama katika shughuli za uvuvi.
Ameongeza kuwa, Kozi hizi zinatarajiwa Kuongeza ufanisi katika shughuli za uvuvi, Kuboresha usalama kwa wavuvi, Kuboresha utunzaji wa mazingira wakati wa shughuli za uvuvi, Kupunguza ajali, vifo, kupotea baharini wakati wa shughuli za uvuvi, Kuongeza uelewa wa sheria, taratibu na miongozo mbalimbali inayohusiana na uvuvi kutoka kwenye mamlaka za ndani na nje ya nchi.
Kampeni hii itafanyika kwa muda wa siku nne kuanzia tarehe 20 hadi 23 Agosti ambapo itahusisha kutembelea wavuvi na viongozi wao pamoja na kutoa elimu katika shule mbalimbali za Lindi.