ELIMU, UWEKEZAJI NA UTEKELEZAJI WA SHERIA NI NGUZO ZA UCHUMI WA BULUU
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, amesema Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu lililofanyika Septemba 7–9, 2026 jijini Dar es Salaam, limejadili maeneo muhimu ya kuzingatiwa katika kuendeleza uchumi wa buluu, ikiwemo matumizi endelevu ya rasilimali za maji, uwekezaji katika teknolojia, elimu na kuongeza uelewa wa wananchi.
Akizungumza Prof. Gurumo alisema majadiliano yalisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za maji kwa manufaa ya kiuchumi huku zikilindwa ili ziendelee kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.
“Tulijadili namna bora ya kutumia maji tuliyonayo na rasilimali zake kwa manufaa ya kiuchumi. Hata hivyo, ni muhimu tukumbuke kuwa tukizidi kulenga uchumi bila kuyatunza maji hayo, rasilimali hizi zinaweza kuisha,” alisema Prof. Gurumo.
Aidha, alisema kongamano hilo lilisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia za kisasa katika taasisi za elimu na mafunzo ya masuala ya bahari, ili kuwaandaa wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kimataifa.
“Tunatakiwa kutoa wahitimu wanaoelewa na kuendana na mahitaji ya soko la ajira la kimataifa. Kutoa mafunzo kwa kutumia vifaa vya zamani ni kuwafanya vijana wetu kuwa wageni wanapoingia kazini. Hali hiyo inaweza kusababisha ajali na uharibifu,” alibainisha.
Prof. Gurumo alisema pia kongamano lilisisitiza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu uchumi wa buluu kuanzia ngazi ya chini, kwa kushirikisha serikali za mitaa, vijiji na halmashauri.
“Bado kuna changamoto ya watu wengi kutojua uchumi wa buluu ni nini, hata wale wanaoishi kando ya maji. Elimu hii inapaswa kutolewa kupitia serikali za mitaa, vijiji na halmashauri kwa kushirikisha wataalamu,” alisisitiza.
