DMI YAZINDUA DAWATI LA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.

10 Sep, 2023
DMI YAZINDUA DAWATI LA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.

 

Uongozi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI) umeelekezwa kusaidia dawati la kupinga ukatili wa kijinsia kutekeleza majukumu yake na kuwa endelevu kwa kutenga bajeti itakayosaidia kuendesha shughuli za dawati, kujenga uelewa wa pamoja kwa jamii nzima ya DMI na kushirikiana na wadau wengine kama polisi ili kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Maelekezo hayo yametolewa leo na Mkurugenzi Msaidizi (Utawala) wa Wizara ya Uchukuzi Ndg. Hamid Mbegu wakati wa uzinduzi wa Dawati la kupinga ukatili wa kijinsia DMI uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo tarehe 8 Septemba 2023.

Mkurugenzi ameipongeza DMI kwa kutekelezaa agizo la Serikalila la kuunda dawati linaloshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia kwani madawati hayo ni vyombo muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika jamii kama ya Chuo cha Bahari yenye watu wa aina tofauti.

Ameongeza kuwa menejimenti ya Chuo inao wajibu wa kulea na kuwezesha dawati hilo kuwa endelevu katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo na wao kama Wizara wataendelea kutoa ushirikiano na kusimamia utekelezaji wa sera hiyo ya kitaifa .

Makamu Mkuu wa Chuo Fedha Utawala na Mipango Dkt.Lucas Mwisila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo amesema kuwa, Uongozi wa Chuo utakua kipaumbele katika kuhakikisha dawati hilo linatekeleza majukumu yake ipasavyo kwani, ukatili wa kijinsia hauathiri sehemu ya kijamii pekee bali hata sehemu ya kiuchumi, hivyo chuo kitajitahidi kuhakikisha jamii yote ya DMI inalindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa Dawati la kijinsia Vyuo vikuu na Vyuo vya kati Bi.Gift Sowoya kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto amesema kuwa dawati hili linalenga kutekeleza majukumu matatu yaani kuzuia, kupambana na kurespond dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia hivyo menejimenti ya chuo isaidie kutatua changamoto zinazowezekana kwa ngazi yao na kwa zile zilizo juu ya uwezo wao kuzifikisha kwenye vyombo husika ili kupata ufumbuzi sahihi.

Mkuu wa kituo cha polisi Buguruni SP. Sarah Kabula amewataka viongozi wa wanafunzi kusambaza uelewa kwa wanafunzi wenzao juu ya uwepo wa dawati hilo na huduma zitolewazo ili kuweza kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia zitakazojitokeza.

 

Mkurugenzi Msaidizi (Utawala) wa Wizara ya Uchukuzi Ndg. Hamid Mbegu (Mgeni rasmi) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Dawati la kupinga ukatili wa kijinsia DMI uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo.

Makamu Mkuu wa Chuo Fedha Utawala na Mipango Dkt.Lucas Mwisila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo wakati wa uzinduzi wa Dawati la kupinga ukatili wa kijinsia.

Mratibu wa Dawati la kijinsia Vyuo vikuu na Vyuo vya kati Bi.Gift Sowoya kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto akizungumzia majukumu ya dawati hilo.

 

Picha ya pamoja ya Viongozi na Waratibu wa dawati la kupinga ukatili wa kijinsia DMI.