DMI YATEMBELEWA NA UJUMBE WA WAFANYABIASHARA TOKA CHINA

16 Dec, 2023
DMI YATEMBELEWA NA UJUMBE WA WAFANYABIASHARA TOKA CHINA

Na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

Ujumbe wa watu 14 wawakilishi wa Kampuni zinazomiliki meli na zinazojihusisha na shughuli za lojistiki za usafirishaji ambao ni wanachama wa Chemba ya Biashara ya Hubei waliopo Shanghai wametembelea Chuo cha Bahari  Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Chuo.

Ujumbe huo toka China uliratibiwa na Mhandisi Gu Jugen, Meneja Ufundi toka Kampuni ya Meli ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China (SNOTASHIP) wapo nchini wakifanya utafiti ili kubaini maeneo ya uwekezaji nchini Tanzania hususan kwenye sekta ya usafirishaji.

Ujumbe huo ulibainisha kuwa ujio wao katika Chuo cha DMI umechangiwa na umuhimu wa huduma zinazotolewa na chuo kwenye biashara zao. Hivyo, wamedhamiria kuwa na mahusiano na DMI katika Kutoa fursa kwa wahitimu wa DMI wa Unahodha na Uhandisi wa Meli kwa madhumuni ya kupewa mafunzo ya vitendo kwenye meli zinazomilikiwa na wafanyabiashara hao.

Pi Kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina kwa wanafunzi na wahitimu wa chuo cha DMI ili kurahisisha mawasiliano na kukuza fursa za ajira kwa vijana wa kitanzania katika kampuni za Kichina zinazojihusisha na usafirishaji na lojistiki zake.

Dkt. Tumaini Gurumo, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam,  ameeleza kuwa ujio wa ujumbe toka Shanghai ni fursa kubwa kwa chuo na nchi kwa ujumla na amewahakikishia kuwa DMI ndiyo chuo pekee  Tanzania na Afrika Mashariki kinachotoa mafunzo ya bahari katika viwango stahiki vya kimataifa.

Aidha, ameeleza kuwa DMI ipo tayari baada ya kujiridhisha na kufuata taratibu kuingia makubaliano ili kuwezesha wanafunzi wa DMI kupata mafunzo ya vitendo ndani ya meli (sea time), ikiwa ni hitaji muhimu ili kuhitimu kozi za ubaharia. Vilevile itakuwa ni fursa maridhawa kwa wahitimu wa DMI kuwa na uhakika wa ajira kwenye kampuni za Kichina zilizowekeza na zitakazo wekeza hapa nchini.