DMI YASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA COSCO SHIPPING S.P.E YA CHINA

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na kampuni kubwa ya usafirishaji wa majini duniani, COSCO Shipping Specialized Carrier Co LTD ya nchini China kwa lengo la kubadilaishana ujuzi na uzoefu.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo tarehe 15 Septemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Jijini Dar es Salaam Kati ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam na Meneja Mkuu wa kampuni ya COSCO na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema ushirikiano huu ni hatua muhimu ya kukuza taaluma ya bahari nchini na kuongeza nafasi za ajira kwa vijana wa Kitanzania kupitia mafunzo ya vitendo na ajira kwenye meli za kimataifa.
“Makubaliano haya ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa buluu (blue economy),Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizi ili kuhakikisha sekta ya baharini inachangia kikamilifu kwenye uchumi wa taifa,” amesema Kahyarara
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam(DMI) Prof. Tumaini Gurumo amesema makubaliano haya yataleta mageuzi makubwa katika mitaala na mafunzo ya wanafunzi, sambamba na kuongeza hadhi ya DMI kuwa kitovu cha mafunzo ya bahari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Tunataka wanafunzi wetu wapate uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira ya kimataifa na kuendeleza taaluma yao kwa kiwango cha juu,” amesema Prof.Gurumo.
Naye Meneja Mkuu wa kampuni ya COSCO Shipping S.P.E Bw. Huang Nan amesisitiza dhamira ya kampuni hiyo kushirikiana na DMI kwa karibu, akibainisha kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza sekta ya usafiri majini na kutoa mchango mkubwa katika soko la ajira la kimataifa.
Ameongeza kuwa kampuni ya COSCO kwa kushirikiana na ile ya SINOTASHIP wako tayari sasa kuipatia nchi ya Tanzania meli kubwa ambayo itakuwa ikisafirisha shehena kutokea hapa nchini kuelekea Mashariki ya mbali hali itakayosaidia kuongeza ushindani na ufanisi wa bandari zetu na kuwaongezea uzoefu wataalamu wetu wa ndani.
Makubaliano haya ya kihistoria yanatarajiwa kuimarisha ubora wa elimu na mafunzo ya bahari, kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza sekta ya baharini na uchumi wa Taifa.