DMI YAENDELEA KUJIVUNIA UMAHIRI WA WAHITIMU WAKE NDANI NA NJE YA TANZANIA
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinaendelea kujivunia mchango mkubwa wa wahitimu wake wanaofanya kazi ndani na nje ya Tanzania, wakionesha ubora, nidhamu na weledi walioupata chuoni.
Akifungua Baraza la Nne la Wahitimu kwenye ukumbi wa chuo tarehe 10 Disemba , Mkuu wa Chuo, Prof. Tumaini Gurumo, aliwapongeza wahitimu kwa hatua yao muhimu ya kitaaluma . Amesisitiza kuwa mafanikio yao yanatokana na juhudi binafsi, nidhamu, pamoja na ubora wa mafunzo yanayotolewa na DMI.
Prof. Gurumo ameeleza kuwa DMI imejijengea nafasi ya kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa elimu inayokidhi viwango vya kimataifa na mahitaji ya sasa ya soko la ajira la baharini. Aidha, amewakumbusha wahitimu kuwa sekta ya bahari inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo ni muhimu kuendelea kujifunza na kuendana na mbinu za kisasa ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo muhimu.
Kupitia ujuzi na mbinu walizojifunza chuoni, wahitimu wa DMI wanaendelea kung’ara katika taasisi za serikali, mashirika binafsi, kampuni za meli na shughuli mbalimbali za baharini duniani, wakithibitisha thamani na umahiri wa mafunzo ya DMI.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DMI Alumni, Nakhodha Grayson Marwa, amesisitiza umuhimu wa wahitimu wa DMI kushiriki mabaraza kama haya. Amesema kuwa fursa hizo huimarisha mitandao ya kitaaluma (professional networking) na kuwawezesha kutoa mawazo chanya yanayosaidia kukiendeleza chuo. Aidha, ameongeza kuwa uzoefu wanaoupata kazini huchangia kuboresha mitaala na kuongeza thamani ya elimu inayotolewa na DMI.
Akihitimisha kongamano hilo, Dkt. Msabaha Mwendapole aliwashukuru washiriki wote kwa mchango wao katika kuendeleza ubora wa taaluma za baharini. Ametaja kuwa ushirikiano wa wahitimu na wadau ni nguzo muhimu ya ukuaji endelevu wa sekta ya bahari.


