WANAFUNZI WA UHANDISI WA MAFUTA NA GESI DMI WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KATIKA MRADI WA MATANGI YA KUHIFADHI MAFUTA BANDARI YA DAR ES SALAAM

18 Aug, 2026
WANAFUNZI WA UHANDISI WA MAFUTA NA GESI DMI WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KATIKA MRADI WA MATANGI YA KUHIFADHI MAFUTA BANDARI YA DAR ES SALAAM


Wanafunzi 135 wa mwaka wa nne wa Shahada ya Uhandisi wa Mafuta na Gesi kutoka Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) wamefanya ziara ya mafunzo katika Mradi wa Matangi ya Kuhifadhi Mafuta uliopo Bandari ya Dar es Salaam chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa lengo la kupata uzoefu wa vitendo kuhusu shughuli na usimamizi wa miradi ya mafuta na gesi.

Ziara hiyo ililenga kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo usimamizi wa miradi ya mafuta na gesi, ikiwemo upangaji, utekelezaji, ufuatiliaji wa miradi pamoja na mifumo ya uhifadhi wa mafuta. Wanafunzi pia walipata fursa ya kujifunza kuhusu viwango vya usalama kazini na matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Meneja Mkuu wa Uhusiano na Masoko wa Bandari ya Dar es Salaam, Bi. Levina Kato, alisema mradi huo una mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya nishati na uchumi wa taifa, huku akiwahimiza wanafunzi kutumia elimu wanayoipata kujenga ubunifu na weledi katika taaluma zao.

Kwa upande wake, Mratibu wa ziara hiyo, Mha. Renatus Kanyambo, alisema ziara hiyo imewawezesha wanafunzi kuunganisha elimu ya darasani na mazingira halisi ya kazi, jambo linalochangia kuwaandaa vyema kwa soko la ajira.

Naye Fabian Masatu mmoja wa wanafunzi walioshiriki ziara hiyo alisema, mafunzo hayo yamewapa uelewa mpana wa namna miradi mikubwa ya mafuta na gesi inavyosimamiwa, huku yakiwawezesha kuona kwa vitendo yale wanayojifunza darasani na kuongeza hamasa katika taaluma yao.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za DMI za kuwapatia wanafunzi uzoefu wa vitendo unaowawezesha kukidhi mahitaji ya sekta ya mafuta na gesi nchini na kimataifa.

 

  •