DMI NA NAMIBIA KUJENGA USHIRIKIANO WA KIMAFUNZO

12 Oct, 2023
DMI NA NAMIBIA KUJENGA USHIRIKIANO WA KIMAFUNZO

Uongozi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam ukiongozwa na Kaimu Mkuu wa Chuo Eng. Juma Kapaya, leo wamekutana na kufanya mazungumzo yenye lengo la kujenga ushirikiano wa kimafunzo na wawakilishi wa Wizara ya Uvuvi na Rasilimali za Bahari (MFMR) kutoka Jamhuri ya Namibia, wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi Bw. Steven Ambabi.

Wakizungumza wakati wa majadiliano hayo kwenye ukumbi wa Chuo cha Bahari Eng.Juma Kapaya alisema kuwa Chuo kimefurahi kuwapokea na kipo tayari kujenga ushirikiano wa kimafunzo na Wizara ya Uvuvi ya Namibia katika kukuza taaluma ya Mabaharia.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Kiufundi Bw. Steven Ambabi kutoka Namibia amesema kuwa, wamefurahishwa na mapokezi ya DMI kwani Wizara yao imelenga kuleta Maofisa 4 wanotarajia kuanza mafunzo yao katika kozi za Cheti cha Umahiri kwa mwaka wa masomo 2023/2024.

Aidha, Bw. Lameck Sondo, Meneja wa Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia kutoka TASAC amesema kuwa Chuo Cha Bahari na TASAC watatoa ushirikiano wa hali ya juu kuhakikisha kuwa wanatimiza lengo la kutoa mafunzo kwa maofisa wa Namibia watakaokidhi vigezo vya kusoma taaluma wanaazozihitaji.

Mbali na mazungumzo, wawakilishi hao walifanikiwa kupitishwa kwenye maeneo muhimu ya mafunzo kwa vitendo yanayotumiwa na wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam.