DMI YAANGAZIA UCHUMI WA BULUU NA AJIRA ZA BAHARIA KATIKA JUKWAA LA KIMATAIFA LA UWEKEZAJI KATIKA BANDARI NA SEKTA YA BAHARI
Ikiwa ni sehemu ya kuonesha utaalamu wake katika sekta ya bahari, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kinashiriki katika Jukwaa na Maonesho ya Kimataifa ya Uwekezaji katika Bandari na Sekta ya Bahari (Ports and Maritime Investment Forum & Exhibition 2026), yanayofanyika tarehe 28–29 Oktoba 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Jukwaa hilo limeandaliwa na Jumuiya ya Usimamizi wa Bandari za Afrika Mashariki na Kusini (PMAESA), likiwakutanisha wadau wa bandari na sekta ya bahari kutoka ndani na nje ya ukanda huu kwa ajili ya kujadili fursa za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya kukuza sekta hiyo.
Katika jukwaa hilo, DMI imewasilisha mada kuhusu Uchumi wa Buluu na Uratibu wa Ubunifu (Blue Economy and Innovation Coordination), pamoja na mada nyingine yenye kichwa “From Training to Employment: Building a Seafarer Pipeline That Works for the Industry”, inayolenga kuunganisha mafunzo na ajira kwa ajili ya kuandaa wataalamu wa ubaharia wenye ujuzi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira katika sekta ya bahari.
Katika eneo la maonesho, washiriki wamepata taarifa kuhusu programu za elimu na mafunzo zinazotolewa na Chuo, zikiwemo Usafiri wa Baharini na Sayansi ya Ubaharia, Uhandisi wa Mitambo ya Meli, Uhandisi wa Mafuta na Gesi, Usafirishaji na Ugavi (Shipping and Logistics), kozi za Cheti cha Umahiri (Certificate of Competency) pamoja na kozi fupi. Aidha, wamepata maelezo kuhusu fursa za ajira, huduma za utafiti na ushauri zinazotolewa na Chuo.
Ushiriki wa DMI katika jukwaa hilo unaendelea kuonesha nafasi ya Chuo katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi kwa ajili ya sekta ya bahari, huku ukifungua fursa mpya za ushirikiano na wadau katika elimu, mafunzo na huduma za kitaalamu za sekta ya bahari, kwa manufaa ya sekta na Taifa kwa ujumla.
