DMI YAELIMISHA JAMII KUHUSU SEKTA YA BAHARI KUPITIA MAONESHO YA HUDUMA ZA MAKTABA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisisitiza umuhimu wa kuandika na kuhifadhi historia, utamaduni na maarifa ya Tanzania ili kuyawezesha vizazi vijavyo kujifunza kupitia vyanzo vilivyoandikwa na Watanzania wenyewe.
Profesa Mkenda aliyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Nne la Kitaifa la Huduma za Maktaba na Tamasha la Vitabu na Usomaji, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika ziara yake kwenye mabanda ya maonesho, Profesa Mkenda alitembelea banda la Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), ambako alipata maelezo kuhusu majukumu ya Chuo, huduma zinazotolewa na Maktaba ya DMI pamoja na vitabu na machapisho yanayohusu sekta ya bahari.
Aidha, Profesa Mkenda alikipongeza Chuo kwa kushiriki maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha jamii, hususan vijana, kuhusu fursa na mchango wa sekta ya bahari katika maendeleo ya taifa.
Maonesho hayo yalifanyika katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, Posta Dar es Salaam, kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba 2026.
