DMI NA NCT WAINGIA MAKUBALIANO YA KUTOA ELIMU NA MAFUNZO YA MABAHARIA WAPISHI
Chuo cha Bahari Dar es salaam na Chuo cha Taifa cha Utalii leo kimefungua fursa mpya ya ajira kwa vijana wa kitanzania na nje ya nchi, kwa kusaini mkataba wa makubaliano ya kutoa Elimu na Mafunzo ya Mabaharia Wapishi Melini, unaolenga kukuza elimu na kuzalisha wataalamu mahiri watakaokidhi vigezo vya kimataifa katika Tasnia ya Bahari na Utalii wa Meli.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es salaam, Dkt.Tumaini Gurumo amesema kuwa ,Chuo cha Bahari kimebobea katika fani za Ubaharia na kina Ithibati ya kimataifa na Chuo cha Utalii kimebobea kwenye mafunzo ya utalii na ukarimu hivyo muunganiko huo utaleta tija ya uchumi wa Bluu nchini kwa kuzalisha wataalamu wenye vigezo.
Amesema, mkataba huu utasaidia juhudi na mikakati ya Serikali kwa kubainisha fursa za ajira ili kuwawezesha vijana wa kitanzania kuzitumia kwa lengo la kujikwamua kiuchumi kupitia fedha za kigeni na ongezeko la mzunguko wa fedha hatimaye kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.
“Tunasikia Uchumi wa Bluu ukipewa kipaumbele, lakini pia tunasikia habari ya ajira kwa vijana imekuwa ikizungumzwa mara, kwa mara, fursa hizi tunaziendeleza kwa kuwawezesha vijana kuzifikia ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Lengo na mikakati yetu ni kusaidia juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kunakuwepo na fursa za ajira kwa vijana” amesema Dkt. Gurumo.
Aidha ameongeza kuwa Kozi ya Mabaharia Wapishi ni miongoni mwa kada saidizi za watumishi wa meli ambapo hadi sasa, mtaala tayari umekwisha pelekwa TASAC kwani wao ndio wanaohusika na utoaji wa vyeti, hivyo kuanzia wiki ijayo dirisha la udahiri wa wanafunzi litafunguliwa kwa vijana wote wanaohitaji kujiunga na kozi hiyo.
“Tunapozungumzia watumishi wa Melini tunakuwa na maeneo matatu muhimu, eneo la kwanza ni Manahodha, Wahandisi na kada saidizi, sasa hizi kada saidizi ndio tumekuwa hatuzifanyii kazi"Ameongeza Dkt.Gurumo
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt.Florian Mtey amesema kuwa Muunganiko huu anauhakika utaenda kuzalisha wahitimu wenye viwango vikubwa sana ambao watafaa kuajiriwa katika mikakati ya Utalii ya Serikali nchini na kunufaika pia na fursa za Utalii wa Meli duniani.
“Kupitia Mashikiano haya, vijana wa Kitanzania wanapata fursa za ajira katika meli za Kitalii zinazosafirisha watalii Duniani, Chuo chetu cha Taifa cha Utalii pamoja na Chuo cha Bahari cha Dar es salaam, tunaingia makubaliano ya kushirikiana kutoa mafunzo kwa mabaharia katika fani ya Upishi na vilevile tutaongeza wigo wa mafunzo katika fani nyingine za ukarimu kwenye meli yatakayowezesha vijana kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.”
“Cheti cha mpishi melini kinahitaji wataalamu waliohitimi kama wapishi waliopata mafunzo ya ubobezi katika tasnia ya bahari na upishi katika hoteli na migahawa , Mpishi wa meli kwa mwaka analipwa dola 65elfu sawa na milioni 150, hii ni fursa kubwa sana kwa vijana wetu wa kitanzania “ Alisema Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
Akishukuru, Makamu Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI) Taaluma Dkt.Lucas Mwisilla amesema, ushirikiano wa vyuo hivyo unaenda kutoa fursa kwa watanzania hivyo, watumishi wanawajibu wa kuhakikisha wanashirikiana na kuandaa mitaala itakayosaidia katika kutoa elimu na mafunzo hayo.
Aidha wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu hassan kwa jitihada za kukuza na kuimarisha utalii na uchumi wa bluu kwa kufungua fursa za Meli kubwa kufika nchini kwa lengo la kufanya utalii.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (kushoto) akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake muda mfupi kabla ya kutiliana saini Makubaliano.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (kushoto aliyekaa) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia aliyekaa)wakitia saini nyaraka za makubaliano (MoU) ya kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani ya mabaharia wapishi .
Mwanasheria wa Chuo cha Bahari DMI (kushoto) na mwanasheria wa Chuo cha Taifa cha Utalii (kulia) wakitia saini mkataba wa makubaliano baina ya taasisi hizo mbili.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (kushoto) Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia) wakikabidhiana nyaraka mara baada ya kutia saini makubaliano (MoU) ya Mashirikiano ya kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani ya upishi.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (kushoto) Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (kulia) katika picha ya pamoja na wanasheria wao mara baada ya kutia saini makubaliano (MoU) ya Mashirikiano ya kutoa mafunzo kwa Mabaharia katika fani ya upishi.
Maafisa wa Chuo cha Bahari DMIwakipiga makofi kupongeza hatua iliyochukuliwa na taasisi hizo mbili.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI) Taaluma Dkt.Lucas Mwisilla akitoa neno la shukurani.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (wa tatu kushoto) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (wa nne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Maafisa wa DMI .
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo (wa tatu kushoto) na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey (wa nne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya Maafisa wa Taasisi hizo mbili mara baada ya kumalizika kwa hafla hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey akitoa neno la ufunguzi wa Hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Utalii.