DHANA YA USHIRIKISHAJI WATUMISHI YAHIMIZWA KUPITIA MABARAZA YA WAFANYAKAZI

22 Mar, 2025
DHANA YA USHIRIKISHAJI WATUMISHI YAHIMIZWA KUPITIA MABARAZA YA WAFANYAKAZI

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo Cha Bahari Dar es salaam wahimizwa umuhimu wa kutekeleza dhana ya ushirikishaji WATUMISHI kupitia mabaraza ili kuleta Amani na utulivu mahala pa kazi unaolenga kuimarisha Uchumi, ufanisi na tija kwa mujibu wa sheria , sera na miongozo mbalimbali ili kuongeza motisha kwa wafanyakazi na kupunguza manung’uniko na migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi.

Ujumbe huo umetolewa na muwezeshaji kutoka ofisi ya kamishna wa kazi, Wizara ya Kazi na Ajira Wakati alipokuwa akitoa mafunzo kuhusu wajibu wa wajumbe wa baraza na miongozo kuhusu mabaraza ya wafanyakazi kwa wajumbe wa baraza la Chuo cha Bahari Dar es salaam wakati wa kikao cha tatu cha baraza la sita la wafanyakazi wa chuo.

Katika mafunzo hayo wajumbe wa baraza la Chuo cha Bahari Dar es salaam waliweza kujifunza mada mbalimbali zikiwemo za nafasi na sifa za wajumbe, maadili ya wajumbe wa baraza pamoja na wajibu wa wajumbe ikiwa ni sehemu ya kukumbushana na kuboresha utendaji kazi wa wajumbe wa baraza kwa mustakabali mzuri wa chuo.

Sambamba na mafunzo hayo wajumbe pia waliweza kupata uelewa kuhusu msongo wa mawazo (stress management) hususani mahala pa kazi na namna ya kukabiliana nao kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kutoka kwa muwezeshaji Elizabeth wa taasisi ya sayansi na teknolojia Vignan tegeta.

Kikao cha tatu cha baraza la sita la wafanyakazi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam kinafanyika kwenye ukumbi wa Stella maris- Bagamoyo kuanzia tarehe 21-22/03/2025 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera, kanuni na miongozo.