CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAM KINAENDELEA KUWA KITOVU CHA UBOBEZI KATIKA FANI YA UCHUMI WA BLUU

27 Jul, 2022
CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAM KINAENDELEA KUWA KITOVU CHA UBOBEZI KATIKA FANI YA UCHUMI WA BLUU

Chuo cha Bahari Dar es Salaam kinaendelea kuwa kitovu cha Ubobezi katika fani ya Uchumi wa Bluu (Blue Economy) katika kanda ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Hayo yamesemwa tarehe 25.07.202 na Mhandisi.Daniel Rukonu katika Warsha fupi ya Maadhimisho ya siku ya Bahari Afrika ambapo Chuo cha Bahari Dar es Salaam kwa pamoja wamekutanika chuoni hapo ili kujadili masuala mbalimbali yahusuyo tasnia ya bahari.

 

Kaimu Mkuu wa Chuo akifungua Warsha fupi ya Maadhimisho ya Siku ya Bahari Afrika katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam

Mhandisi Daniel Rukonu alisema Chuo cha Bahari Dar es Salaam pamoja na wadau wengine wa sekta ya Bahari, wanaadhimisha na kuunga mkono jitihada za Umoja wa Africa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuilinda Bahari na rasilimali zake.

“Africa tunayoitaka (Agenda 2063) ni ya kuweka kipaumbele katika maendeleo ya kiuchumi ambayo yanategemea zaidi Uchumi wa Bahari (Uchumi wa Bluu) ambapo Chuo cha Bahari Dar es Salaam ni sehemu muhimu na mchangiaji wa kutoa mafunzo na watalaam barani mwetu Tangu 1978”, Mhandisi Daniel Rukonu alisema

 

Mhandisi Daniel Rukonu akiwasilisha Mada katika Maadhimisho ya siku ya Bahari Afrika

Katika kutambua mchango mkubwa utokanao na tasnia ya bahari,Chuo cha Bahari Dar es Salaam kinatoa mafunzo sahihi yahusuyo bahari na uchumi wa bluu yakiwemo Mafunzo ya Usafirishaji kwa Njia ya Maji (Maritime Transport), Sayansi ya Usafiri wa Majini (Nautical Science), Utafiti na Utafutaji wa Mafuta (Oil and Gas Exploration), Ujenzi wa Meli (Naval Architecture and Ship Construction), Uhandisi wa Mitambo ya Meli (Marine Engineering), Lojistiki na Usafirishaji (Shipping and Logistics) na Ubaharia ( Proffesional Seamanship)

Aidha Chuo cha Bahari Dar es Salaam kama Chuo cha umma kina nafasi kubwa katika kuyabeba malengo ya nchi kwa kusaidia kukua kwa sekta za bahari kupitia Uchumi wa buluu inapotoa mafunzo,tafiti na huduma za jamii kwa kuwa jamii kubwa ya watanzania na Africa tumezungukwa na maji ambapo yatupasa sasa kuona uchumi wa bahari kama fursa mbichi ili itusaidie kuleta maendeleo endelevu,ukuaji wa uchumi na ustawi jamii inayotegemea rasiliamali za bahari.

Katika kuhakikisha hayo yanakuwa halisi,Chuo cha Bahari Dar es Salaam kina jukumu kubwa la kufundisha wabobezi na wafanyakazi katika sekta mbalimbali zinazonufaika na Uchumi wa bahari na bahari kuu na kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza wigo wa shughuli za uchumi kuvuka nchi kavu kuelekea bahari. Kipekee uchumi wa bahari ni wa uhakika na utasaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wenyewe na kuongeza wigo wa ajira na ustawi wa jamii.

 

Watumishi wakifuatlia mada katika Maadhimisho ya siku ya Bahari Afrika