CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) NA CHUO KIKUU CHA BAHARI CHA DALIAN CHA UCHINA(DMU) WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

17 Jun, 2026
CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) NA CHUO KIKUU CHA BAHARI CHA DALIAN CHA UCHINA(DMU) WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Bahari cha Dalian Maritime University (DMU) cha nchini China lengo la makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu ya bahari.

Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, alieleza umuhimu wa ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili na mafanikio yanayotarajiwa kupatikana kupitia mahusiano hayo kwa miaka mingi ijayo. Alisema kuwa miongoni mwa manufaa ya ushirikiano huo ni kubadilishana uzoefu kwa wanafunzi na kupeana uzoefu kwa watumishi wa vyuo hivyo.

  Kwa upande  wake Mkuu wa chuo cha DMU Profesa Shan Hongjun alieleza dhamira ya Dalian Maritime University ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya taasisi hizo mbili na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano katika maendeleo ya elimu ya bahari, utafiti na ubunifu. Aliongeza kuwa mahusiano haya ni kielelezo cha mahusiano mazuri baina ya Uchina na Tanzania.

Makubaliano hayo yalisainiwa tarehe 4 Juni 2026, katika kampasi ya chuo hicho jijini Dalian nchini China, baada kutia saini Mkuu wa chuo cha DMU  alisema kuwa makubaliano  hayo yatakayowezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za pamoja zikiwemo kubadilishana wanafunzi na wahadhiri, kufanya tafiti za pamoja za kisayansi, kuandaa programu za pamoja za kitaaluma, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika maandalizi ya mitaala na mafunzo ya kitaalamu yanayokidhi mahitaji ya sekta ya usafirishaji majini.

kusainiwa kwa makubaliano hayo ni mwanzo mpya katika kuanzisha na kutekeleza miradi ya pamoja yenye ubora wa hali ya juu kwa kutumia rasilimali za kielimu zilizopo katika taasisi zote mbili pia itasaidia kuongeza uwezo wa wahadhiri na wanafunzi, kuimarisha tafiti za pamoja na kuendeleza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta ya bahari.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu ya bahari, utafiti, ubunifu na utekelezaji wa ajenda ya Uchumi wa Buluu nchini Tanzania na China, huku yakifungua fursa mpya za ushirikiano wa kimataifa kwa wanafunzi na watumishi wa taasisi hizo.