CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM CHAINGIA MAKUBALIANO NA DANAOS SHIPPING COMPANY LIMITED
Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimeingia makubaliano ya ushirikiano (MOU) na kampuni ya meli Danaos Shipping Company Limited kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano katika utoaji elimu na mafunzo ya Ubaharia. Makubaliano haya yamefanyika katika ukumbi wa DMI kati ya Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo na Mkurugenzi Mkuu wa Danaos Shipping Company Limited tawi la Zanzibar Bw. Mzee Ali Mzee tarehe 07 Februari, 2024.
Makubaliano hayo yalishuhudiwa na Mwakilishi wa Danaos Shipping Company Limited Kapt. Stylianos Petronios na Menejimenti ya DMI.
Mkuu wa chuo cha Bahari Dar es Salaama Dkt. Gurumo amesema kuwa makubaliano haya ya miaka mitano (5) ni muhimu kwa maendeleo ya elimu ya mabaharia na sekta ya bahari nchini.
"Kampuni ya Danaos yenye makao makuu yake mjini Piraeus nchini Ugiriki ina meli zaidi ya 80 barani Africa hivyo ni fursa kwa chuo cha DMI kupata nafasi zaidi za mafunzo ya vitendo melini kwa wanafunzi hasa wale wa uhandisi wa meli na unahodha." Alisema Dkt. Gurumo.
Dkt. Gurumo aliongeza kuwa makubaliano haya yatafungua wigo kwa watanzania wengi kupata ajira zenye staha na kuinua kipato cha familia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu kutoka Danaos Shipping Company Limited tawi la Zanzibar Bw. Mzee Ali Mzee amesema kuwa makubaliano hayo yana manufaa makubwa kwa watanzania na yatawezesha wanafunzi wengi zaidi wa DMI kwenda katika meli za Danaos kupata mafunzo kwa vitendo hivyo kunufaika kiujuzi zaidi.
Aliongeza na kusema kampuni ya Danaos imeajiri mabaharia wa kitanzania 700 ambao wanaleta fedha za kigeni nchini hivyo kuchangia vilivyo katika kukuza uchumi wa nchi.