CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) KIMESAINI HATI YA MASHIRIKIANO NA SHIRIKA LA KITAIFA LA MASUALA YA BAHARI LA MUUNGANO WA COMORO (ANAM)

04 Sep, 2024
CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI) KIMESAINI HATI YA MASHIRIKIANO NA SHIRIKA LA KITAIFA LA MASUALA YA BAHARI LA MUUNGANO WA COMORO (ANAM)

Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesaini hati ya mashirikiano na Shirika la Kitaifa la Masuala ya Bahari la Muungano wa Comoro (ANAM) katika masuala ya elimu, mafunzo, tafiti na ushauri  kuhusuu masuala ya bahari kwa lengo la kubadilishana uzoefu.

Akizungumza leo Septemba 3, 2024 Mkuu wa Chuo cha DMI Dkt.Tumaini Gurumo amesema ushirikiano wa Tanzania na Comoro katika masuala mbalimbali ya kibiashara umeanza muda mrefu na kwa upande wa masuala ya bahari wameamua kuingia makubaliano hayo kwani komoro ni kisiwa chenye matumizi mengi ya maji ambayo yanahitaji usimamizi.

Amesema kuwa komoro wamesajili meli nyingi takribani 300, lakini hawana uwezo mzuri wa kuzisimamia hivyo wakipatiwa mafunzo na DMI kuhusu masuala ya  sekta ya bahari yatawawezesha kuwasaidia katika kuziendesha meli hizo.

 "Watanzania wengi wapo Comoro wanafanya biashara na Wacomoro wapo Tanzania wanafanya biashara pia, makubaliano haya tunayosaini lengo kuu ni kuhakikisha tunakuwa karibu katika kujenga rasilimali watu iliyobobea kwenye masuala ya bahari kwenye nchi hizi ili ziwanufaishe vijana wetu kupitia mafunzo bora yanayotolewa DMI katika kuziendea fursa zilizopo baharini" Amesema Dkt. Tumaini

Ameongeza kuwa Komoro haina watu wengi lakini wamezungukwa na maji kwa kiasi kikubwa,  matumizi ya maji yanahitaji watu wenye weledi na usimamizi sahihi wa meli zilizosajiliwa, matamanio ya mashirikiano haya ni kuona wenzetu wanaitumia bahari kwa ufanisi kupitia mashirikiano ya kubadilishana uzoefu.

"Tunakwenda kushirikiana kuhakikisha tunapata rasilimali watu yenye weledi kupitia chuo hichi kilichobobea kwenye utoaji wa elimu, mafunzo na  kwa kufanya  tafiti mbalimbali ili kujua jinsi gani tunaondoa changamoto zilizopo,"amesema Dkt.Gurumo.

Naye Mkurugenzi wa ANAM  Bw. Mohamed Dahalani  amesema asilimia 80 ya wafanyabiashara kutoka Comoro wanakuja Tanzania  kuchukua  mizigo kwa kutumia meli kutokana na uwezo mzuri wa usimamizi wa bahari  uliopo kuliko komoro, makubaliano haya yataleta tija kwani wanafunzi wanaotoka Komoro  baada ya kuhitimu DMI wamekuwa wakifanya vizuri katika masuala ya usimamizi na uendeshaji wa bandari nchini humo.

Aidha ameongeza mbali na kupiga hatua katika suala la usajili wa meli bado wamekuwa wakipoteza biashara nyingi kutokana na ukosefu wa usimamizi wa bahari na meli hivyo kupitia ushirikiano huu utawawezesha kukabiliana na changamoto hizo katika kukuza uchumi wa komoro.