BILIONI MBILI ZATUMIKA KUNUNULIA MTAMBO WA KUFUNDISHIA CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI)

07 Nov, 2023
BILIONI MBILI ZATUMIKA KUNUNULIA MTAMBO WA KUFUNDISHIA CHUO CHA BAHARI DAR ES SALAAM (DMI)

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi imetumia zaidi ya shilingi bilioni mbili nukta tano(2,744,106,712.35) kununulia Mtambo (Crane Simulator ) wa kisasa wa kufundishia kwa ajili ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)

Mkuu wa chuo hicho Dokta Tumaini Gurumo amesema Mtambo (Crane Simulator) huo utasaidia kufundishia wanafunzi kwa vitendo na kuongeza thamani ya elimu inayotolewa katika chuo hicho pekee hapa nchini.

“Mtambo huu unasaidia kufundishia katika kozi ambazo utendaji kazi wake ni maeneo ya Bandari, Viwandani na Migodini. Zaidi ya Shilingi bilioni mbili nukta tano imetumika kununulia Mtambo huu mpaka kufunga hapa chuoni” alisema Dkt. Tumaini.

Tumaini ailongeza kuwa mtambo huo utasaidia sana kwenye mafunzo kwa vitendo, kuongeza uzalishaji wa wanataalamu wenye ujuzi wa viwango vya juu kwani mtambo huu unalenga kujengea uwezo wanafunzi utakaosaidia kuongeza tija katika maeneo mbalimbali.

Elinathan Blasius Mtaalamu wa Mtambo huo na Mkufunzi wa Chuo cha Bahari Dar es salaam amesema kuwa mtambo huo wa kisasa ni muhimu kwa wanafunzi kwani utasaidia kupata elimu ya kuendesha mitambo mabalimbali.

“ Kwa kila mtambo huu una mada zaidi ya kumi hivyo kila mwanafunzi atapata elimu ambayo itamsaidia kuendesha mitambo mikubwa na midogo”Alisema Elinathan.

Kwa upande wake Mwalimu Leonard Mwesiga amesema kuwa mtambo huo ni muhimu sana kwa chuo hicho kwani unaweza kufundishia wanafunzi zaidi ya masomo sita na mwanafunzi akihitimu katika masomo hayo ataweza kuendesha mitambo ya aina yoyote katika sekta ya Bandari, Viwandani na Migodini.