TANZANIA KUPITIA WANAFUNZI WA DMI YAIBUKA KIDEDEA MAFUNZO KWA VITENDO MELINI KOREA YA KUSINI
Wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam walioshiriki mafunzo kwa vitendo melini katika Chuo cha Bahari na Teknolojia ya Uvuvi cha Korea ya Kusini wameibuka na ushindi wa Timu bora ya mwaka 2024 kwa kuzingatia uwezo wa Kitaaluma na ushirikiano katika eneo la Unahodha wa meli na Uhandisi wa meli kati ya nchi 13 zilizoshiriki mafunzo hayo. Kati ya vijana hawa wapo waliopata tuzo binafsi za Uongozi bora na kuwa mabaharia wanafunzi wa mfano bora wa kuigwa.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya wanafunzi hao kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam Dkt. Tumaini Gurumo amesema kuwa, kutokana na uhaba wa Meli za Mafunzo hapa Nchini, Chuo kiliingia mashirikiano na Chuo cha KIMFT kilichopo Korea ya Kusini ili kubadilishana uzoefu wa mafunzo yanayohusu Bahari.
Dkt. Tumaini ameongeza kuwa ushirikiano baina ya vyuo hivyo umewawezesha wanafunzi kushiriki mafunzo kwa vitendo melini yanayowaongezea uwezo na ufanisi katika utendaji kazi.
“Tunashukuru sana Serikali ya Korea ya Kusini kupitia chuo cha KIMFT kwa kuwezesha wanafunzi wetu kupata Mafunzo kwa vitendo. Tunashukuru pia Ubalozi wetu wa Korea Kusini kwa ushirikiano wa karibu katika kutafuta fursa za uchumi wa buluu ” Alisema Tumaini.
Mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam Nahodha. Andrea Matilya amesema kuwa Chuo kinajivunia kuwa na Mashirikiano na Nchi zinazosaidia kuchukua wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo kwani, inasaidia katika kuzalisha rasilimali watu kwenye sekta ya Bahari wenye uwezo na ushindani wa kufanya kazi kwenye meli kubwa na ndogo za ndani na nje ya nchi.
Ahamadi Selele ni miongoni mwa wanafunzi watano waliopata mafunzo hayo amesema kuwa wamekutana na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali kama vile Korea Kusini, Singapore, Kenya, Filipino na Taiwani hivyo wamejifunza mengi kuhusu kushirikiana na wafanyakazi wengine wa mataifa mbalimbali kwenye Meli.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi Bi. Honarata Mrema ameshukuru uongozi wa Chuo cha DMI kutoa fursa kwa wanafunzi kupata nafasi ya kujifunza katika nchi nyingine.
Tanzania imekua nchi bora kati ya nchi 13 zilizoshiriki mafunzo kwa vitendo melini katika Chuo cha KIMFT kupitia wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).