CHUO CHA BAHARI (DMI) KUANDAA KONGAMANO LA TATU LA UCHUMI WA BULUU

16 Mar, 2024
CHUO CHA BAHARI (DMI) KUANDAA KONGAMANO LA TATU LA UCHUMI WA BULUU

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dkt. Tumaini Gurumo ametoa wito kwa Watanzania kushirikiana na DMI katika kufanikisha kongamano la tatu la Kimataifa la Uchumi wa Buluu linalotarajiwa kufanyika tarehe 4 na 5 Julai 2024 katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Rai hiyo ameitoa leo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa mikutano wa DMI , Dkt. Tumaini amesema anaomba ushirikiano wa taasisi zote za Serikali hususani wizara zinazosimamia shughuli mbalimbali za Uchumi wa Buluu, Wadau wa Elimu, Sekta binafsi kama kampuni za Meli na Usafirishaji Pamoja na Taasisi za fedha.

Dkt.Tumaini amesema kuwa Kongamano hili linafanywa na DMI kwa kushirikiana na Chuo cha Regional Maritime University (RMU) kilichopo nchini Ghana kwa lengo la kukutanisha wadau wa Uchumi wa Buluu ili kujadiliana na kubadilishana uzoefu katika kukuza dhana ya Uchumi wa Buluu Afrika.

" Kongamano hili linaandaliwa na DMI kwasababu ndio Chuo pekee katika nchi hii kilichopewa dhamana ya kufundisha masuala yanayohusu Bahari kwa mapana yake. Hivyo basi, majukumu yake hayawezi kutenganishwa na uchumi wa Buluu" Alisema Dkt.Tumaini

Dkt. Tumaini amesema mbali na kongamano hilo kuchochea tafiti ambalo ni jukumu la Chuo lakini pia, linalenga kutoa elimu ya masuala ya Uchumi wa Buluu kwa Watanzania ili kuwawezesha kuziendea fursa zinazopatikana katika eneo hilo kama kilimo cha mwani, gesi na mafuta, uvuvi na ufugaji samaki, utalii na mambo mengine.

Aidha, amesema kuwa katika kongamano hilo watakuwepo watoa mada kutoka Nchi mbalimbali ikiwemo Gambia, Ghana, Kenya na Tanzania ambao tayari wamejitokeza. Pia, kutakuwa na washiriki kutoka nje ya Afrika ikiwemo Korea, China, Italy, Marekani na Denmark.

Pia, Mkuu wa Chuo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha ushirikiano na Mataifa mengine unaosaidia taasisi kama ya DMI kunufaika nao.

Kongamano hili limebebwa na kauli mbiu ambayo inalenga kufungamanisha Uchumi wa buluu na mambo matatu ya Usalama na Ulinzi baharini, Maendeleo ya kiteknolojia Pamoja na Mabadiliko ya hali ya hewa.

Ikumbukwe kuwa, Kongamano hili ni matokeo ya Makangomano mawili yaliyowahi kufanywa na DMI Mwaka 2022 na 2023.